MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya
ya Mbulu Mkoani Manyara wametakiwa kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
ili waweze kupatiwa matibabu pindi wakiugua wao na wategemezi wao watano.
Hayo yamesemwa na Ofisa matekelezo
wa mfuko huo Haji Mpeta wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani
wa halmashauri hiyo kilichofanyika juzi katika ukumbi wa halmashauri ya
wilayani hiyo.
Mpeta alisema kuwa kwa mujibu wa
sheria kila diwani nchini anapaswa kujiunga na mfuko huo wa bima ya afya ambapo
atahudumiwa yeye na wategemezi wake watano wa kisheria.
Alisema mfuko huo hutoa aina 623 ya dawa
zilizosajiliwa na mamlaka ya chakula na dawa nchini na pia hugharimia dawa za
magonjwa ya kansa,moyo na figo na wagojwa watakaolazwa hospitalini.
Alisema mfuko huo pia hugharamikia
upasuaji mdogo,mkubwa na wakitaalamu lakini haugharamikii magonjwa ya kifua
kikuu,ukoma na dawa za kufubaza virusi vya ukimwi (ARV) kwani magonjwa hayo
yamepewa kipaumbele na Taifa.
“Pamoja na hayo lakini mfuko wa
bima ya afya haugharamikii tendo la kuvunja sheria ikiwemo kutaka kujitoa uhai
kwa kujinyonga,kunywa sumu au kujichoma kisu au kuathirika kwa kutumia dawa
zilizopigwa marufuku,” alisema Mpeta.
Hata hivyo,madiwani hao
walikubalina na suala la kujiunga kwenye mfuko huo kwa kuchangia japokuwa
wamebakiza kipindi cha takribani miaka michache kabla ya kumaliza kipindi chao
mwaka 2015.
Baadhi ya madiwani hao na kata zao
kwenye mabano Valerian Gidshang (Endagikot) na Paulo Sulle (Daudi) walidai kuwa
watajiunga kwenye mfuko huo kwani una manufaa makubwa na wataishawishi jamii
ijiunge na mfuko huo.