WANAWAKE WAJAWAZITO KUTOKA JAMII YA WAFUGAJI WAJENGEWA ZAHANATI

WANAWAKE  kutoka jamii ya kifugaji waishio katika kijiji cha Ekenywa wilayani Arumeru ,wameondokana na  adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili ya ukosefu wa kituo cha Afya baada ya shirika lisilokuwa la kiserikali la SOS  children’s kujitolea kuwajengea zahanati itakayowasaidia kupata huduma wakati wa kujifungua.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zahanati hiyo   mganga mkuu wa mkoa wa Arusha,Dkt Frida Maruti alisema zahanati hiyo imekuja wakati mwafaka na itakuwa mkombozi kwa wananchi waishio maeneo ya wafugaji, kwani itasaidia sana katika kupunguza vifo vya akina mama na wajawazito .
Aidha alisema,hatua ya uwepo wa kituo hicho itaondoa changamoto kwa akinamama kutembea umbali mrefu kusaka huduma hiyo  kwa lengo la kujifungua ,kwani kabla ya hapo wengi wao walikuwa wakijifungua majumbani hali ambayo ilikuwa ikihatarisha maisha yao.
Pamoja na kulipongeza shirika hilo kwa msaada wa zahanati hiyo,alitoa wito kwa wakinamama kuhakikisha wanaitumia zahanati hiyo kwa kupata matibabu na kuacha ile tabia iliyojengeka kwa jamii hiyo kujifungulia majumbani.
Pia alitoa wito kwa shirika hilo pamoja na wadau wengine wa afya kuhakikisha wanajitolea zaidi katika kuboresha zahanati hiyo ili iwe na wodi ya kulaza wagonjwa,hata hivyo aliitaka serikali kusaidia kuleta wataalamu wa huduma ya mama na mtoto.
N aye mkurugenzi wa Sos Children’s,Rita Kahurananga alisema kuwa shirika hilo limejikita zaidi katika kuwahuduamia watoto na akinamama na kwamba uzinduzi wa kituo hicho unalenga kuwasogezea huduma akina mama na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Alisema ujenzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa miradi mingi ya vituo vilivyopo katika mikoa ya Dar es salaam,Zanzibar na Arusha.
Kwa upande wa mganga mkuu wa kituo hicho,dkt Frenk Lisso alisema kuwa zahanati hiyo itawasaidia pia watoto zaidi 150 wanaofadhiliwa na shirika hilo la kimataifa la Sos ambalo limejikita kufadhili miradi inayomsaidia  mama na mtoto.
Alisema awali kabla ya zahanati hiyo walipata shida sana jinsi ya kuwapa huduma watoto wanaolelewa katika kituo hicho cha Sos kwani baadhi ya watoto hao wanamaambukizi ya virusi vya vvu pamoja na watoto ambao wametelekezwa na wazazi wao kutokana na maisha magumu wakiwa na umri mdogo.

 
  

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post