UNYAMA WA KUTISHA ARUMERU,FAMILIA 5 ZAKOSA MAHALI PA KUISHI

Baadhi ya wakazi waliobomolewa nyumba zao wakiwa wamekaa nje
UNYAMA wa kutisha umejitokeza katika kijiji cha Sing”isi wilayani Arumeru Mashariki mkoani Arusha mara baada ya familia tano kubomolewa  nyumba zao  kwa amri ya wawekezaji  wa kigeni wanaomiliki  mashamba makubwa  wilayani humo  hali ambayo imepelekea  familia hizo kulala nje.

Wananchi hao wanaishi karibu na shamba kubwa la wawekezaji wa kigeni liitwalo Mito miwili ambapo hivi karibuni lilivamiwa na wananchi wilayani humo kwa madai kwamba wanataka wamilikishwe ardhi yao.



Hatahivo,familia hizo zenye wakazi zaidi ya 30 zimeiangukia serikali na kuitaka iingilie kati sakata hilo kwa madai kwamba wanateseka kwa kuishi na hofu ,kukosa chakula sanjari na watoto wao kutohudhuria masomo mashuleni.

Tukio hilo la kinyama linadaiwa kutokea hivi karibuni majira ya saa 6.30 usiku ambapo wakiwa wamelala watu ambao wametajwa kuwa ni madalali wa wawekezaji wa kigeni wanaomiliki mashamba makubwa walivamia katika makazi yao na kisha kuwatoa nje kabla kabla ya kuanza kubomoa nyumba zao.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo juzi wakazi hao walisema kwamba watu hao mara baada ya kuwatoa nje waliwakusanya na kisha kuwafungia katika chumba kimoja na kisha kuanza kubomoa nyumba zao.

Mzee,Fataeli Macha pamoja na mkewe Hellen Macha walisimulia kwamba wao ni wakazi halali wa maeneo hayo tangu miaka ya sitini huku wakisimulia kwamba mbali na kubomolewa nyumba zao waliporwa mali mbalimbali kama simu,radio,fedha  na mali mbalimbali na kisha kutokomea kusikojulikana.

Kwa nyakati tofauti wakazi hao walisema kwamba watu hao kabla ya kuanza kubomoa nyumba zao waliwakuwa wakiwatamkia maneno ya kwamba kwanini wamekataa kulipwa fidia ili waondoke katika makazi hayo na kisha wwaachie wawekezaji.

“Walikuwa wanatuambia ya kwamba kwanini tumekataa kulipwa fidia ili tuhame katika makazi haya na tuwaachie wawekezaji”walisema kwa nyakati tofauti

Naye,Rehema Mohamed na Amina Idd walisema kwamba watu hao walikuwa wamevalia kofia na makoti meusi ambapo baadhi yao walipigwa na vitu vizito kabla ya zoezi la kubomolewa nyumba zao.

Hatahivyo,walimtaja mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Kileo kwamba ndiye dalali wa wawekezaji wa kigeni wanaomiliki mashamba makubwa yaliyopo karibu na makazi yao kwamba amekuwa akiwashawishi wao kupokea fedha za fidia ili wapishe lakini wamekataa.


 Walienda mbali zaidi na kusisitiza ya kuwa mkuu wa wilaya ya Arumeru alifika kuwatembelea na kisha kuwatafutia baadhi yao nyumba za wageni ili wakahifadhiwe huku wakiitaja taasisi ya Tumaini Foundation kwamba imewasaidia chakula na msaada wa mashuka.

 Mkuu wa wilaya ya Arumeru,Jeremba Munasa alipohojiwa juu ya tukio hilo alisema kwamba serikali bado inafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka waliofanya vitendo hivyo.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post