Rwanda wiki hii imetofautina na ripoti ya wasimamizi walioteuliwa na
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) kusimamia
mwenendo wa kesi inayomkabili Mchungaji Jean Uwinkindi juu ya madai ya
kukosekana kwa fedha za kugharimia huduma za kisheria, huku Shirika la
Kupigania Haki za Binadamu, Human Rights Watch likidai kwamba
kumefanyika uhalifu wa kivita wakati wa kumkamata kiongozi wa zamani wa
Libya, Muammar Gaddafi.
ICTR
Wataka ripoti ya waliohamishiwa Ufaransa: Jumatatu wiki hii, Rwanda
imerudia malalamiko yake mjini The Hague, Uholanzi kwa kucheleweshwa
kusikilizwa kwa kesi mbili zilizohamishiwa kwenda kusikilizwa nchini
Ufaransa na Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa mwaka 2007 na kutoa wito
wa kutolewa kwa ripoti kamili juu ya suala hilo. Kesi hizo zinawahusu
Padre Wenceslas Munyeshyaka na Mkuu wa zamani wa mkoa, Laurent
Bucyibaruta.
Rwanda, ICTR wapingana juu ya kugharimia kesi ya Uwinkindi: Rwanda
Jumanne wiki hii imetofautina na ripoti ya wasimamizi walioteuliwa na
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) kusimamia
mwenendo wa kesi inayomkabili Mchungaji Jean Uwinkindi juu ya madai ya
kukosekana kwa fedha za kugharimia huduma za kisheria.Wakati wasimamizi
wa kesi hiyo wamedai katika ripoti yao kwamba hakuna fedha za kugharimia
upelelezi na upatikanaji wa mashahidi wa utetezi, wakuu wa Rwanda
amekanusha madai hayo kwa kusema kuwa hakuna ukosefu wa fedha kwa ajili
ya kazi hiyo.
ICC
Kesi ya Bemba yaendelea kusikilizwa: Kesi ya utetezi ya Kiongozi wa
zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean
Pierre Bemba imeendelea usikilizwa Jumatatu wiki hii kwa kupata ushahidi
toka kwa shahidi wa sita ambaye alikuwa mlinzi wa zamani katika kikosi
cha walinzi wa Rais katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR). Bemba
anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita
unaodaiwa kufanywa na askari wake kati ya 2002 na 2003 katika Jamhuri ya
Afrika ya Kati.
Wadai kufanyika kwa uhalifu wa kivita wakati wa kumkamata Gaddafi:
Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Human
Rights Watch iliyotolewa Jumatano wiki hii imedai kwamba wanamgambo
waasi nchini Libya walifanya mauaji ya halaiki ya watu Oktoba 20, 2011
katika mji wa Sirte, wakati wa kumtia mbaroni kiongozi wa zamani wa
Libya Muammar Gaddafi ambaye pia aliuawa. Ripoti hiyo inatilia shaka
taarifa ya serikali ya Libya kwamba Gaddafi aliuawa katika uwanja wa
mapambano na siyo baada ya kutiwa mbaroni.
Shirika la Amnesty International lataka Al-Senuss ahamishiwe ICC:
Shirika la Amnesty International Alhamisi wiki hii lilitoa wito kwa
mamlaka ya Libya kumkabidhi mara moja Abdullah al-Senussi kwenye
mahakama ya ICC ili akabiliane na mashitaka ya uhalifu dhidi ya
binadamu.Afisa mmoja alidai kwamba mwaka mmoja baada ya kumalizika kwa
machafuko nchini humo waathirika wa ukiukwaji mkubwa wa uhalifu dhidi ya
binadamu wa utawala wa zamani na pia wapinzani wao hawajatendewa haki.
WIKI IJAYO
ICC
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma: Kesi ya utetezi ya kiongozi wa
zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean
Pierre Bemba itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Oktoba 22. Bemba
anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita
unaodaiwa kufanywa na askari wake kati ya 2002 na 2003 katika Jamhuri ya
Afrika ya Kati.