RWANDA YAPINGANA NA ICTR GHARAMA ZA UTETEZI KESI YA UWINKINDI,WADAI KUFANYIKA UHALIFU WA KIVITA WAKATI WA KUMTIA MBARONI GADDAFI


 Rwanda wiki hii imetofautina na ripoti ya wasimamizi walioteuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) kusimamia mwenendo wa kesi inayomkabili Mchungaji Jean Uwinkindi juu ya madai ya kukosekana kwa fedha za kugharimia huduma za kisheria, huku Shirika la Kupigania Haki za Binadamu, Human Rights Watch likidai kwamba kumefanyika uhalifu wa kivita wakati wa kumkamata kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi.

ICTR
Wataka ripoti ya waliohamishiwa Ufaransa: Jumatatu wiki hii, Rwanda imerudia malalamiko yake mjini The Hague, Uholanzi kwa kucheleweshwa kusikilizwa kwa kesi mbili zilizohamishiwa kwenda kusikilizwa nchini Ufaransa na Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa mwaka 2007 na kutoa wito wa kutolewa kwa ripoti kamili juu ya suala hilo. Kesi hizo zinawahusu Padre Wenceslas Munyeshyaka na Mkuu wa zamani wa mkoa, Laurent Bucyibaruta.
Rwanda, ICTR wapingana juu ya kugharimia kesi ya Uwinkindi:  Rwanda Jumanne wiki hii imetofautina na ripoti ya wasimamizi walioteuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) kusimamia mwenendo wa kesi inayomkabili Mchungaji Jean Uwinkindi juu ya madai ya kukosekana kwa fedha za kugharimia huduma za kisheria.Wakati wasimamizi wa kesi hiyo wamedai katika ripoti yao kwamba hakuna fedha za kugharimia upelelezi na upatikanaji wa mashahidi wa utetezi, wakuu wa Rwanda amekanusha madai hayo kwa kusema kuwa hakuna ukosefu wa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
ICC
Kesi ya Bemba yaendelea kusikilizwa: Kesi ya utetezi ya Kiongozi wa zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean Pierre Bemba imeendelea usikilizwa Jumatatu wiki hii kwa kupata ushahidi toka kwa shahidi wa sita ambaye alikuwa mlinzi wa zamani katika kikosi cha walinzi wa Rais katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR). Bemba anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na askari wake kati ya 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wadai kufanyika kwa uhalifu wa kivita wakati wa kumkamata Gaddafi: Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch iliyotolewa Jumatano wiki hii imedai kwamba wanamgambo waasi nchini Libya walifanya mauaji ya halaiki ya watu Oktoba 20, 2011 katika mji wa Sirte, wakati wa kumtia mbaroni kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi ambaye pia aliuawa. Ripoti hiyo inatilia shaka taarifa ya serikali ya Libya kwamba Gaddafi aliuawa katika uwanja wa mapambano na siyo baada ya kutiwa mbaroni.
Shirika la Amnesty International lataka Al-Senuss ahamishiwe ICC: Shirika la Amnesty International Alhamisi wiki hii lilitoa wito kwa mamlaka ya Libya kumkabidhi mara moja Abdullah al-Senussi kwenye mahakama ya ICC ili akabiliane na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu.Afisa mmoja alidai kwamba mwaka mmoja baada ya kumalizika kwa machafuko nchini humo waathirika wa ukiukwaji mkubwa wa uhalifu dhidi ya binadamu wa utawala wa zamani na pia wapinzani wao hawajatendewa haki.
WIKI IJAYO 
ICC
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma: Kesi ya utetezi ya kiongozi wa zamani wa waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean Pierre Bemba itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Oktoba 22. Bemba anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na askari wake kati ya 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post