Utata umezidi kuibuka katika Bunge Maalumu la Katiba kutokana na
kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya
Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.
Utata huo, umebainika katika Kamati kadhaa siku
moja tangu wajumbe wa Bunge hilo waanze kujadili sura ya kwanza na ya
sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
muundo wake.
Jana Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa
Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini
uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana
na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha,
alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa
ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa.
Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana
hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano,
Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali
kadhalika.
Nahodha alisema baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.
Kauli hiyo ya Nahodha inapingana na kauli ya
Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad ambaye jana alisema hati
hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka
bungeni Dodoma.
“Ile hati ya Muungano ipo Dar es Salaam, lakini
tunahofia kuileta maana inaweza kupotea kwani ipo moja tu, sasa ambacho
tutakifanya inaweza kutolewa nakala na kuthibitishwa na mawakili na
ikaja nakala hapa Dodoma iwapo wajumbe wanahitaji,” alisema Hamad.
Nahodha alipoelezwa juu ya majibu ya Katibu wa
Bunge kuwa hati hiyo ipo Dar es Salaam, alishikwa na mshangao na kusema
wanamuomba Katibu huyo, aiwasilishe kama ipo.
Sheria za Muungano
Katika hatua nyingine, Sheria Namba 22 ya 1964 ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuridhia Muungano nayo haijulikani ilipo.
Baadhi ya wajumbe katika Kamati Namba 2 walidokeza
kuwa, walipohoji kuhusu sheria hiyo walisomewa kitabu cha aliyewahi
kuwa Mwanasheria wa Zanzibar, Abdul Jumbe na kuambiwa kwamba picha za
ukumbusho zipo.