Mafundi wa Kampuni ya Oilcom wakiangalia mabaki ya lori la kampuni hiyo
lililochanika baada ya kulipuka kwa tanki lake wakati likichomewa katika
eneo la Tabata Relini, jijini Dar es Salaam
Taharuki ya aina yake ilitokea jana eneo la Tabata Relini kwenye
yadi ya malori ya Kampuni ya Oilcom baada ya kutokea kishindo kikubwa
kilichotokana na kupasuka kwa tanki la mafuta.
Tukio hilo lililotokea saa 11 jioni, lilizua hofu
miongoni mwa wakazi na wafanyakazi wa eneo hilo, na lilitokana na
hitilafu ya kiufundi wakati wa kulitengeneza tanki hilo.
Mashuhuda wa tukio hilo lililojeruhi watu watatu
waliliambia Mwananchi kuwa mlipuko huo ulitokea wakati fundi akichomea
sehemu ya tanki katika karakana ya magari ya kampuni hiyo.
“Kuna fundi alikuwa juu ya lori akipima mifuniko
na chini alikuwepo dereva wa lori hilo na fundi mwingine wa kuchomea
vyuma akichomea, wote walikuwa wakiendelea na kazi.
“Dereva wa lori hilo alikuwa akimuelekeza fundi
sehemu ya kuchomea na ghafla ukatokea mlipuko mkubwa,” alisema Omari
Wenge, fundi katika karakana hiyo.
Alisema mlipuko huo ulimtupa chini fundi aliyekuwa juu ya tanki na kulikosababisha aumie usoni na sehemu za kifuani.
Shuhuda huyo alisema dereva na fundi wa kuchomea,
waliumizwa sehemu mbalimbali za mwili kwa kupigwa na vipande vya mabati
ya tanki na kichwa cha gari hilo.
Majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika
Hospitali ya Amana kwa matibabu zaidi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni Camillus Wambura alisema kuwa hakuwa amepata
taarifa zozote za ajali hiyo hivyo angetujulisha pindi angezipata.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya
wafanyakazi wa karakana hiyo wakipewa huduma ya kwanza baada ya kuzimia
kwa mshtuko huku wengine wakiweweseka kwa hofu.
Kichwa cha lori hilo kilichakazwa na mlipuko huo
ambao moja ya mabati yanayoligawa tanki hilo yalitupwa upande wa pili wa
Barabara ya Mandela.
Sehemu ya juu ya mbele ya lori hilo, ilitupwa juu
ya paa la moja ya majengo ya karakana hiyo huku chini zikiwa zimetapakaa
nyaraka na mabaki mengine ya sehemu ya mbele ya lori hilo.
Naye mmoja wa mashuhuda, Boniface Msisi
aliyekuwemo ndani ya karakana hiyo, alisema hali ndani ya eneo hilo
ilibadilika ghafla huku kila mfanyakazi akitafuta mlango wa kutokea.