CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepitisha mpango mkakati wake wa kuelekea kushika dola mwaka 2015 kwa kumega madaraka ya makao makuu katika kanda kumi.
Maazimio hayo yalipitishwa na Kamati Kuu (CC) juzi kwa agenda moja kubwa ambayo ni kupitisha mpango mkakati wa mwaka 2013 ili kushinda chaguzi zote kuanzia serikali za vitongoji, vijiji na mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza na wajumbe wa kikao cha dharura cha Baraza Kuu jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kuwa mpango mkakati huo umelenga kufanya mabadiliko ya uongozi kuanzia ngazi ya taifa kwenda katika majimbo na kukipanga upya chama hicho kwa mustakabali wa taifa.
“Mtakumbuka kwamba wakati tunakianzisha chama chetu, tulizungumzia sera ya majimbo na kuainisha kazi zake…sasa tumeanza kupanga kazi zenyewe kwa kugawa majukumu katika kanda kumi.
“Tunataka tuishi vile tunavyosema kwa kuwa katika miaka mingi ya kuwa chini ya uongozi wa serikali ya CCM, wananchi wamekuwa wakiamriwa mambo yao na kundi dogo la watu wanaojikusanya sehemu moja ya nchi, hilo kwetu si mfano bora wa uongozi,” alisema.
Mbowe aliongeza kuwa katika miaka 20 ya kuhimili misukosuko ya kisiasa chama hicho kimejifunza mengi na sasa kiko tayari kushika dola ndio maana wameanza kugawa majukumu kwa wananchi kupitia uongozi wa kikanda.
Alisema kuwa wamejiandaa kwa mashambulizi ya aina zote na sasa jukumu kubwa la kila kanda litakuwa ni kuhakikisha kila mwananchi anaiunga mkono CHADEMA katika eneo atakalokuwa.
Mwenyekiti huyo alitaja kanda hizo na mikoa husika kuwa ni Kanda ya Ziwa Magaharibi (Mwanza, Geita, Kagera), Ziwa Mashariki (Mara, Simiyu, Shinyanga), Ziwa Magharibi (Kigoma, Tabora, Katavi) na Kati (Singida, Dodoma, Morogoro).
Zingine ni Kata za Nyanda za Juuu Kusini (Mbeya, Ruvuma, Iringa), Kusini (Lindi na Mtwara), Mashariki (Pwani, Dar es Salaam na Tanga), Kaskazini (Kilimanjaro, Manyara, Arusha), Pemba na Kanda ya Unguja.
Mbowe alisema katika kuhakikisha vikosi hivyo vinafanya kazi zake vizuri, kila kanda itajengewa ofisi, kununuliwa magari, pikipiki na vifaa vyote vya ofisini na za mikutano.
“Lengo la mkakati huo pia ni kuhakikisha CHADEMA inasimama katika chaguzi zote bila kupingwa…tunataka CCM ndiyo ipingwe katika chaguzi na hili tutalifanikisha,” aliongeza.
Katika suala zima la Muungano, Mbowe alisema uwepo wa serikali tatu hauepukiki kwa kuwa tayari Tanzania Visiwani wameshakuwa na serikali yao hivyo ni jukumu la Watanzania Bara kupata serikali ya Tanganyika na kisha kuwepo na serikali ndogo ya Muungano.
Alisema serikali tatu inawezekana ikiwa viongozi wataacha unafiki wa kusema muungano utavunjika huku tayari wakitoa uhuru wa Zanzibar kuwa na Rais, bendera na wimbo wao ya taifa.
Tunawaunga mkono wenzetu Wazanzibar katika kupigania uhuru kamili na kwa sasa sisi ndio tunaoonekana wa ajabu kushindwa kuuliza serikali ya Tanganyika,” alisema.
Mbowe pia aligusia tume huru ya uchaguzi akisema serikali ihakikishe Watanzania wanapata tume hiyo kwa kuwa tayari hata viongozi wa chombo hicho wameshatoa maoni na kutaka wapewe uhuru wa kufanya kazi.
Alisema serikali kama inafikiri kuwa CHADEMA itaingia katika uchaguzi wa 2015 ikiwa chini ya tume iliyopo sasa watakuwa wanajidanganya na badala yake watalazimisha upatikanaji wa tume hiyo.
Wailiza CCM Kagera
Katika hatua nyingine chama hicho kimeiliza CCM katika uchaguzi mdogo wa vijiji na vitongoji uliofanyika wilayani Muleba mkoani Kagera Jumapili iliyopita.
Licha ya wilaya ya Mulebe yenye majimbo mawili ya uchaguzi kusini na kaskazini yakiwa chini ya CCM, CHADEMA imeweza kunyakuwa viti vingi vilivyokuwa vikishikiliwa na chama hicho tawala.
Katika uchaguzi huo CHADEMA ilinyakuwa vijiji vitatu kati ya vitano katika jimbo la Muleba Kusini linaloongozwa na Prof. Anna Tibaijuka ambavyo ni Kasenyi, Kabunga na Ihangilo.
CHADEMA pia imechukua vitongoji sita vya CCM kati ya 12 vilivyofanya uchaguzi. Vitongoji hivyo ni Nyamagojo, Mushumba, Nyakabingo, Kyamyorwa, Katanda na Kyogoma.
Katika Jimbo la Muleba Kaskazini, linaloshikiliwa na Charles Mwijage, CCM ilipoteza vijiji viwili vya Katoke na Kahumulo kati ya vitano vilivyofanya uchaguzi huku vitongoji vinne vya Rundu, Kalee, Lwanganilo na Kituvi vikiangukia kwa CHADEMA.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka Muleba, Katibu wa Baraza la Vijana wa Taifa (BAVICHA), Robert Rwegasira, alisema wamepata ushindi huo kutokana na wananchi kuanza kuwaamini.
Mafanikio hayo yametokana na hamasa ya vuguvugu la mabadiliko la CHADEMA (M4C) ambalo lilifanyika katika mkoa wa Kagera Novemba mwaka jana.
Katika jimbo la Muleba Kusini, CHADEMA ingeweza kupata viti vya vitongoji zaidi ya idadi iliyopata kwani walisimamisha wagombea tisa kati ya 12 huku nafasi tatu wakiwaachia CUF na NCCR-Mageuzi ambao hawakuambulia chochote.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia