Rais Jakaya Kikwete akiwa katika
Picha ya Pamoja na wachezaji wa Timu ya Taifa , Taifa Stars, viongozi
wa Wizara ya Habari, Vijana ,Utamaduni na Michezo na Viongozi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Rais wa Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo amekutana na timu ya
Taifa (Taifa stars) kwa lengo la kuitia moyo katika mechi ijayo kati
yake na timu ya Moroco ikiwa ni harakati za Tanzania kutafuta tiketi ya
kucheza fainali za kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2014.
Rais Kikwete ameiambia timu
hiyo kuwa ina uwezo mkubwa wa kusonga mbele kutokana na uwezo mkubwa
waliouonesha katika mchezo wao dhidi ya Gambia ambapo walifanikiwa
kupata ushindi wa bao 2-0.
“Maadamu mara ya kwanza
mliwashinda Gambia, hakikisheni pia mnapata ushindi dhidi ya Moroco,
mkishinda tunafurahi sana na mkishindwa tunanyong’onyea sana,” amesema
Rais Kikwete.
Aidha amempongeza kocha wa
timu hiyo Kim Poulsen pamoja na Kamati ya Taifa ya ushindi ya Taifa
stars kwa kuisaidia timu hiyo kiasi cha shilingi milioni 30 ikiwa ni
mkakati wa kuiongezea nguvu kwa hatua iliyofikia na kuwataka wachezaji
kujituma ili kuwafurahisha watanzania ambao hivi sasa wanaipenda timu
yao ya Taifa.
Nae Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Fenera Mukangara amesema Serikali itaendelea
kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo nchini ili kuondoa
changamoto zinazoikabili timu hiyo.
Kwa upande wake Kocha Poulsen,
amemshukuru Rais Kikwete kwa kuwakaribisha na kuwatia moyo ambapo
ameahidi kuifundisha vizuri timu hiyo ili kuhakikisha kuwa wanapata
ushindi.
Akizungumza kwa niaba ya
wachezaji wenzake kaptaini wa timu hiyo Juma Kaseja amemshukuru Rais
Kikwete na kuahidi kujituma kwenye mazoezi na hatimaye kuibuka washindi
kwenye mechi zijazo.
Taifa stars ambayo inakamata nafasi ya pili katika kundi C inatarajia kucheza ugenini na Morocco mnamo Juni 7 mwaka huu.