WAFUGAJI wa kabila Barbaig waishio porini katika pori
lililopo eneo la Maramboi,kijiji cha Mdorii wilayani Babati mkoani
Manyara,wamemlalamikia mwekezaji wa
Kifaransa anayedaiwa kumega eneo lao kibabe na kufanya makazi ya kudumu ikiwemo
kujenga hotel ya kitalii bila kuwashirikisha huku akitumia walinzi wake
kuwanyanyasa kwa kuwachapa viboko na kuwafungulia kesi mbalimbali polisi ili
wayakimbie makazi yao.
Aidha wameeleza kuwa licha ya kupeleka malalamiko yao
mara kadhaa kwenye vyombo vya dola na viongozi mbalimbali eneo hilo,wamekuwa
hawasikilizwi zaidi ya kupuuzwa na baadhi yao kujikuta wakigeuziwa kibao kwa
kubambikizwa kesi mbalimbali katika kituo cha polisi Minjingu.
Mwekezaji huyo aliyetajwa kwa jina la Nicholaus Negre(38)
anadaiwa kuviweka mfukoni vyombo vya dola,waziri wa Mali asili na Utalii,Hamis
Kagasheki pamoja na viongozi mbalimbali waliopo eneo hilo kiasi cha kushindwa kusema
lolote juu yake na kumwacha aendelee kutenda atakavyo kwa wafugaji hao bila
kuchukuliwa hatua za kisheria,huku akimweleza mwandishi wa habari kuwa hata
habari hizi zikimfikia waziri Kagasheki hatishiki kwani ,waziri hiyo
anamfahamu.
Wafugaji hao wamedai kuwa licha ya kushinda rufaa yao
katika kesi ya msingi walioshitakiwa baraza la Ardhi na nyumba na mwekezaji huyo , bado vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa
na walinzi wa mwekezaji huyo vinaendelea na hawana pa kukimbilia baada ya
viongozi mbalimbali katika wilaya ya Babati na mkoa kudaiwa kuwekwa mfukoni na
Mwakezaji huyo.
Mmoja wa wafugaji hao,Assecheck Yonas(68) alisema kuwa
katika eneo hilo la Maramboi lenye ukubwa wa hekari 45 walianza kuishi tangu
miaka ya 1960 wakiendesha shughuli zao za ufugaji na uwindaji na kwamba ilipofika
mwaka 2008 waliletewa hati ya wito katika
mahakama hiyo wakidaiwa kuvamia eneo hilo .
Aidha katika mwenendo huo wa kesi wafugaji hao,wakiwakilishwa na wakili, John
Materu wa kampuni ya uwakili ya Materu ya jijini Arusha,walishindwa mara mbili
lakini mwaka 2012 walikata rufaa kwa majaji watatu katika mahakama kuu ya
Arusha na ilipofika tarehe 15.3.2013 hukumu
ilitolewa kuwa wameshinda rufaa.
Mahakama hiyo ilijiridhisha kuwa hapakuwa na muhtasari wa kikao cha kijiji
kilichoketi na kukubaliana kulitwaa eneo hilo kwa mwekezaji,ambapo mahakama
iliamuru wafugaji hao kuendelea kuishi katika eneo hilo pasipo na shaka yoyote.
Kwa upande wa mwekezaji huyo,Nicholaus akizungumza na
mwandishi wa habari alisema kuwa alipatiwa eneo hilo kihalali baada ya kuomba kwa uongozi wa kijiji mwaka
2008 na kuonyeshwa eneo hilo lenye ukubwa hekari
45 .
‘’mimi nilikuja kama mwekezaji na nikaomba eneo kwa
kijiji nikaonyeshwa hakari 45kwa ajili ya kujenga na kuendeleza utalii’’alisema
Nicholaus
Aidha alikiri kuwakuta wafugaji hao na alipohoji uhalali
wa wafugaji hao ndani ya eneo hilo alijibiwa kuwa hao ni watu wa kuondoka na watahama muda wowote,hakuna sababu ya kuwa
na mashaka na uwepo wao.
Hata hivyo alisisitiza kwa kusema kuwa haogopi kiongozi
yoyote wa ngazi yoyote hapa nchini,na kueleza kuwa hata wakienda kulalamika kwa
waziri wa maliasili na utalii ,Hamis Kagasheki hawatasaidiwa chochote kwani
wanafahamiana vizuri na waziri huyo .
‘’mimi siogopi mbunge wala polisi ana kiongozi yoyote
hata kama wataenda kwa Kagasheki hawataambilia chochote kagasheki ananifahamu
vizuri’’alisisitiza Nicholaus kwa kujiamini.
Hata hivyo katika hali ya kushangaza alisema kuwa
yeye hana mgogoro na wafugaji hao ila
wenye mgogoro huo ni uongozi wa kijiji hicho pamoja na Jumuiya ya hifadhi ya
wanyama pori Burunge,(WMA Burunge)ambao alidai ndio wamiliki na wasimamizi wa
maeneo ya hifadhi ya wanyama pori.
Jitihada
za kumpata waziri Kagasheki kupitia simu yake ya kiganjani
zilishindikana kwani mara zote alipokuwa akitafutwa alidai yupo kwenye
kikao cha bunge dodoma.
Naye mwenyekiti wa kijiji hicho ,Erasto Belela alisema
kuwa pamoja na mahakama ya rufaa kuwapa ushindi ila kijiji kina taratibu zake
na kimetenga eneo la ekari tatu kwa kila
mfugaji ili ahame katika eneo hilo na kumpisha mwekezaji ,hata hivyo alikanusha
suala la kuwekwa mfukoni yeye na wenzake na mwekezaji huyo.