BREAKING NEWS

Wednesday, May 22, 2013

WANAUME WAMETAKIWA KUBADILI MTAZAMO KUHUSU UGONJWA WA FISTULA



Msanii mahiri wa kizazi kipya Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA (pichani) ambae ni Balozi wa Chapa Vodacom amesema hadhi na heshima ya mwanaume katika jamii  itakuwa na uzito mbele ya uso wa jamii kwa wao kuwa tayari kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili jamii na wala si vinginevyo.
Balozi huyo maarufu kwa jina la Mwana FA ametoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati wa kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu fistula iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square kuelekea siku ya fistula dunaini Mei 23. Kampeni hiyo inadhaminiwa na kampuni ya Vodacom na Vodafone ya Uingereza ikiihusisha mikoa mbalimbali.
Balozi huyo amesema ni wazi kwamba wanaume wamekuwa wamiliki wa maamuzi katika jamii huku wakitajwa kuwa nguzo ya familia lakini sifa hizo na mamlaka hayo yatakuwa na dosari kubwa iwapo hawatokuwa pia mstari wa mbele katika kuhakikisha jamii inapata suluhisho la matatizo.
Balozi huyo ambae alikuwa akielimisha wakazi wa mji wa Dodoma kuhusu fistula, amesema fistula sio tatizo kama ambavyo inaweza kufikiriwa kwa kuwa jambo gumu lingekuwa namna ya kupata matibabu na uwezo wa kugharamia matibabu  hayo.
“Hakuna mwanamke ambaye anapata fistula bila ya mwanaume kuwa chanzo kwa kuwa ndio tunaowapa ujauzito wake zetu, hivyo sio vema na haki kwa mwanaume kumkimbia mkewe au kumtenga mwanamke eti tu kwa sababu mwanamke huyo ana tatizo la fistula.”Alisema Balozi huyo
 “Nawaomba sana wakazi wa Dodoma hasa wanaume tubadili mtazamo tulinao juu ya fistula kwa kutambua kwamba sisi ndio chanzo cha wanawake kupata fistula lakini zaidi ni kwamba hilo sio tatizo kwa kuwa tatizo ni lile ambalo halina suluhisho, fistula inatibika na tena inatibika bila malipo kwa ufadhili wa Vodacom na Vodafone, nini zaidi tunachohitaji katika hili?.”Alihoji Mwana FA
Amesema uamuzi alioufanya kukubali kutembea nchi nzima kuhamasisha akina baba kuondokana na dhana hasi juu ya fistula ikiwemo kuhusisha tatizo hilo na ushirikina au laana na hivyo kuwakimbia wake zao au kushiriki kwa namna yoyote katika kuwanyanyapaa wanawake wenye tatizo la fistula ulikuwa ni mgumu lakini alikubali kwa kuwa anaamini jamii itamuelewa.
“Haikuwa kazi rahisi kwangu kukubali kuongoza msafara huu lakini baada ya kutathmini na kuona jinsi akina mama wanavyoteseka kwa tatizo hili nilijihisi mwepesi kukubali kuzunguka kila kona kuongea na wanaume wenzangu kuwahamasisha kuwa tayari kwa pamoja kuunga mkono kampeni hii ili kufikia lengo la Vodacom la kumaliza tatizo la fistula ifikapo mwaka 2016 .”Aliongeza
“Iwapo kuna mtu(Vodacom)amejitolea kutoa suluhisho la tatizo kwa kulipia nauli, chakula, malazi na matibabu hatuwezi tena kusema fistula ni tatizo,kikwazo pekee tulichonayo hapa ni kuhakikisha kila mmoja anafikiwa na taarifa na ujumbe huu.”Aliongeza
Mwana FA amekuwa chachu katika kampeni hii kwa namna ambavyo ushawishi wake umewezesha kwa kiasi kikubwa ujumbe wa fistula kuwaingia wanaume huku baadhi yao wakimuahidi kumuunga mkono kwa dhati.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ummy Mwalimu alisema si haki kuendelea kuwaacha wanawake wakiteseka wakati fursa ya kuwawezesha kupata matibabu ipo na hivyo ameitaka jamii kuiunga mkono kampeni hiyo na kuitumia ipasavyo.
“Tunaishukuru Vodacom kwa kuweka mfumo wezeshi kwa jamii kupata elimu ya fistula na pia kuwawezesha wanawake kupata matibabu ya fistula bila malipo, naomba wakazi wa mji wa Dodoma na nchi nzima tuitumie fursa hii na tuwe mabalozi kwa wenzetu.”
“Vodacom inafanya kazi kubwa sana kusaidia jamii hapa nchini. Kamwe hatutoona aibu kuipongeza ndani na nje ya Bunge kwa kazi hiyo kubwa na znuri wanayoifanya ikiwemo kampeni hii ya fistula na ufadhili inaotoa kwa wanawake kupata matibabu bila malipo.”Alongeza Ummy
Amesema kuwa jamii lazima ione na kutambua kuwa mwanamke ana wajibu wa kuwa na afya njema ili nae aweze kushiriki katika shughuli za kijamii na za kiuchumi na hivyo kuchangia maendeleo ya kaya na jamii anamoishi.
Naibu Waziri huyo amekiri kuwepo kwa hali ya unyanyapaa kwa jamii kwa wanawake wanaokabiliwa na matatizo ya fistula hali ambayo amesema ni lazima ibadilike hasa wakati huu ambapo fursa za matibabu bila malipo zipo ikiwepo na kuahidi kuibeba ajenda hiyo kwa nguvu zake zote.
Vodacom hutumia wastani wa Sh 700,000 hadi 900,000 kulipia matibabu ya mgonjwa mmoja wa fistula kwenye hospitali ya CCBRT.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Said Mtanda amesema anatambua vema tatizo la fistula na athari zake kwa wanawake wazazi na kwamba pamoja na ukweli kuwa amekuwa akichukua juhudi binafsi katika kusaidia wanawake wenye fistula lakini sasa anaibeba kampeni hiyo na kuiwasilisha katika kamati yake ili kuipa nguvu rasmi za kibunge.
“Naahidi kuwa nitawasilsiha kwenye kamati yangu ujumbe wa kamati hii ikiwa ni pamoja na kuiomba nguvu za kamati hiyo na kuwashawishi wajumbe kuubeba ujumbe wa kampeni hii ndani ya Bunge ikiwemo wakati wa shughuli rasmi za kamati na Bunge kwa ujumla.”Alisema Mtanda 
Kampeni hiyo iliyolenga kuifikia mikoa mbalimbali itamaliza safari yake Mei 23 jijini Dar es salaam siku ya fistula Duniani.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates