CHADEMA WANASA MIKAKATI YA CCM KINANA KUMUONDOA LISSU BUNGENI
Posted by
woinde
on
Friday, May 31, 2013
in
|
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA UMMA
KINANA, CCM WANAPANGA NJAMA ZA KUMVUA LISSU UBUNGE MAHAKAMANI!!!
Dar es Salaam, 31 Mei 2013...
Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelaani vikali njama za Katibu
Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana kufufua kesi ya
uchaguzi dhidi ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na
Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Mh. Tundu Lissu. Katika taarifa
yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr. Wilbroad Slaa
amedai kwamba CHADEMA imekamata nyaraka zinazoonyesha kwamba Katibu Mkuu
wa CCM Kinana amewaelekeza waliowakuwa mawakili wa makada wa CCM
waliomfungulia Mh. Lissu kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge
katika Jimbo la Singida Mashariki mwaka 2010 wafungue rufaa katika
Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda
ya Dodoma iliyotupilia mbali kesi ya makada hao wa CCM dhidi ya Lissu.
Kesi ya Mahakama Kuu ilitupiliwa mbali tarehe 27 Aprili mwaka jana.
Dr.
Slaa alisema kwamba lengo la njama za Kinana na CCM ni kuhakikisha
kwamba Mh. Lissu anafutiwa Ubunge ili asiweze kushiriki katika mchakato
wa Katiba Mpya kama mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba litakalojadili na
kupitisha rasimu ya Katiba Mpya baadaye mwaka huu. Dr. Slaa alisema:
“Kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni na Mbunge, Mheshimiwa Lissu amekuwa mwiba mkali kwa CCM
na Serikali yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Amefumbua
macho ya mamilioni ya Watanzania kuhusu masuala makubwa ya kikatiba na
kisheria kwa hoja zake Bungeni. Uelewa wake mpana wa masuala hayo na wa
Kanuni za Bunge umekuwa kikwazo kikubwa kwa CCM na Serikali yake pamoja
na uongozi wa Bunge kupitisha mambo yao kinyume cha sheria, Kanuni za
Bunge na maslahi ya nchi yetu. Uwepo wake ndani ya Bunge na ujasiri wake
katika kutetea hoja mbali mbali umemzuia Spika wa Bunge na uongozi
mzima wa Bunge kuwaonea Wabunge wa Upinzani na hasa CHADEMA. Mtu huyu
amekuwa adui mkubwa wa CCM ndio maana Kinana anataka aondolewe Bungeni
ili asiwepo kabisa katika mjadala wa Katiba Mpya Bungeni.”
Kwa
mujibu wa Dr. Slaa, mara baada ya Mh. Lissu kuwasilisha hotuba ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria
tarehe 3 mwezi huu ambapo aliishambulia Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
CCM kwa kuvuruga mchakato wa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa
lengo la kuhakikisha Mabaraza hayo yanakuwa ya wanachama wa CCM tu,
Kinana alimwita wakili wa kujitegemea Godfrey Wassonga wa kampuni ya
mawakili ya Wassonga Associates Advocates ya mjini Dodoma na kumwelekeza
afungue rufaa dhidi ya Lissu katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
haraka iwezekanavyo. Siku nne baadaye yaani tarehe 7 Mei, 2013, Wakili
Wassonga alifungua rufaa hiyo katika Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa
ya Tanzania mjini Dodoma.
Ijapokuwa
rufaa hiyo inaonyesha kufunguliwa na Shabani Itambu Selema na Paschal
Marcel Hallu waliokuwa walalamikaji katika kesi iliyotupwa na Mahakama
Kuu, Dr. Slaa alidai kwamba watu hao hawahusiki kwa namna yoyote ile na
kufunguliwa kwa rufaa hiyo.
“CCM
na mawakili wao wanawatumia tu wanakijiji hawa bila hata kuwapa taarifa
au kuwashirikisha kwa namna nyingine yoyote. Huyu Shabani Itambu Selema
amekula kiapo mahakamani Dodoma kwamba yeye na mwenzake ambaye bado ni
Katibu Kata wa CCM huko kwao, hawakuambiwa chochote juu ya kufunguliwa
kwa rufaa hiyo. Hawakutoa maagizo yoyote kwa Wakili Wassonga kufungua
rufaa kwa niaba yao dhidi ya Lissu; hawajamruhusu Wakili huyo kupinga
maamuzi ya Mahakama Kuu iliyoridhika kwamba uchaguzi wa Mbunge Lissu
ulikuwa halali; hawajamlipa Wakili Wassonga kwa ajili hiyo. Huyu Wakili
anafunguaje kesi au rufaa bila kuambiwa au kulipwa na ‘wateja’ wake?
Kama huku sio kukosa maadili ya kiuwakili ni kitu gani?”, amehoji Dr.
Slaa.
Kuhusu
ushiriki wa Kinana katika sakata hilo, Dr. Slaa alisema kwamba mara
baada ya rufaa hiyo kufunguliwa, Wakili Wassonga alimwandikia Katibu
Mkuu huyo wa CCM barua yenye kumbu kumbu Na. NO/KM/CCM/01/2013 kwa ajili
ya “MADAI YA MALIPO YA AWALI YA SHAURI LA RUFAA KESI YA UCHAGUZI JIMBO
LA SINGIDA MASHARIKI SHABANI ITAMBU SELEMA NA MWENZAKE DHIDI YA MH.
TUNDU LISSU.” Barua hiyo inamkumbusha Kinana juu ya ‘makubaliano’ kati
ya Wassonga Associates Advocates na CCM kuhusu kusimamia kesi ya
wanachama hao wa CCM dhidi ya Mh. Lissu ambayo baadae ilitupiliwa mbali
na Mahakama Kuu.
“Baada
ya shauri husika nilipata maelekezo kutoka kwa wanasheria wa CCM kwamba
tukate rufaa Mahakama ya Rufaa kazi ambayo tumekamilisha.” Wakili
Wassonga anamweleza Kinana “... katika shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa
na CCM Singida Mkoa na hawakumalizia malipo.” Barua hiyo imeambatana na
hati ya madai ya malipo (invoice) kwa ajili ya ‘malipo ya awali’ ya
shilingi milioni mbili.
Dr.
Slaa alidai kwamba kazi ya Lissu na wabunge wa CHADEMA ndani ya Bunge
inawatisha CCM na Serikali yake ndio maana sasa Kinana anataka Lissu
aenguliwe kwa kutumia Mahakama ya Rufaa ya Tanzania. “CCM inatapatapa,
Bungeni hapakaliki kwa sababu ya hoja za Lissu na Wabunge wengine wa
CHADEMA. Kila siku Bunge linaahirishwa ili kukwepa mijadala mikubwa juu
ya matukio muhimu yanayoisibu nchi yetu.
Njama
za kuizima CHADEMA kwa kuipunguzia muda wa kuzungumza Bungeni
zimeshindikana; mikakati ya kuvuruga hoja za CHADEMA kwa kuingilia
hotuba za Kambi Rasmi ya Upinzani na kutaka sehemu za hotuba hizo
zifutwe zimegonga mwamba; vitisho vya Spika Makinda na Naibu Spika
Ndugai kuwasimamisha wabunge wetu hazijafua dafu. Sasa tuna taarifa
kwamba Kinana anataka kuwahonga majaji ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
mamilioni ya fedha ili wamfutie Kamanda wetu Lissu ubunge. Naye
atashindwa pia.”
Akizungumzia
hati ya kiapo ya Shabani Itambu Selema ambaye alihama CCM na kujiunga
na CHADEMA baada ya kesi yao kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu mwaka
jana, Dr. Slaa amesema:
“Tutaishangaa
sana Mahakama ya Rufaa kama itaisikiliza rufaa hiyo hata baada ya
aliyekuwa mhusika wa kesi ya msingi kusema kwa kiapo kwamba yeye na
mwenzake hawajakata rufaa bali ni mambo ya Kinana na CCM yake!”
Dr.
Slaa alisema itakuwa ajabu kwa Mahakama ya Rufaa kusikiliza rufaa
iliyofunguliwa zaidi ya mwaka mmoja tangu Mahakama Kuu ilipotupilia
mbali kesi ya msingi. “Kwa mujibu wa kifungu cha 115 cha Sheria ya
Uchaguzi, Sura ya 343, Mahakama ya Rufaa inatakiwa kusikiliza rufaa
dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu
rufaa ilipofunguliwa. Huyu Kinana na CCM yake wamesubiri mwaka umepita
tangu Mahakama Kuu ilipokataa kufuta matokeo ya Lissu ndio wafungue
rufaa. Kama huku sio kukanyaga spirit ya Sheria hiyo ni kitu gani?”,
amehoji Dr. Slaa.
Aliongeza
kuwa katika kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Mh. Godbless Lema
aliyekuwa anashtakiwa na wanaCCM pia, Mahakama ya Rufaa ilipiga
marufuku wapiga kura ambao hawakunyimwa haki zao za kupiga kura kufungua
malalamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
“Hata
wino wa Mahakama ya Rufaa katika hukumu ya Lema haujakauka Kinana na
CCM yake wanataka Mahakama ya Rufaa iyale matapishi yake kwa kusikiliza
rufaa ya wapiga kura wanaodai kwa kiapo kwamba walielekezwa na wakubwa
wao katika CCM kufungua kesi iliyokataliwa na Mahakama Kuu na sasa rufaa
imefunguliwa kwa maelekezo ya Kinana bila hata wao kujulishwa au
kushirikishwa kwa namna yoyote ile," amesema Dkt. Slaa.
Dr.
Slaa alisema kwamba rufaa ya sasa inathibitisha kauli inayodaiwa
kutolewa na Rais Jakaya Kikwete juu ya Tundu Lissu wakati wa kampeni za
Uchaguzi Mkuu uliopita ambapo Kikwete alidaiwa kuwaambia wanaCCM mjini
Singida kwamba ni afadhali Dr. Slaa achaguliwe kuwa Rais kuliko Tundu
Lissu kuwa Mbunge.
“Kwa
kazi zake ndani na nje ya Bunge Lissu amethibitisha umahiri na uzalendo
wake kwa Tanzania na kwa chama chetu. Ametetea wabunge na viongozi wetu
dhidi ya njama za CCM kuwachafua kwa kuwafungulia mashtaka ya uongo
mahakamani; ametetea Watanzania kila mahali nchini, na ameelimisha
wananchi kwa hoja zake Bungeni. Ni mmoja wa Wabunge hodari, jasiri na
wachapa kazi katika Bunge hili. Huyu ndiye Mbunge ambaye Kinana na CCM
wanataka aondolewe Bungeni kwa mbinu za kishetani za aina hii.
Hatutakubali na tunawataka Watanzania wasikubali!”
Rufaa
dhidi ya Lissu bado haijapatiwa namba ya usajili licha ya kwamba
imeshalipiwa ada ya kuifungulia na tayari imeshapokelewa na Masjala
Ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, Dodoma. Aidha, rufaa hiyo
haijapangiwa majaji wa kuisikiliza wala tarehe ya kusikilizwa kwake
haijapangwa.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia