Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na
masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko
kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha. Tukio hilo la kigaidi limesababisha mtu mmoja
kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa.
Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu
katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu
wake.
Rais Kikwete ameagiza
vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho
kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote
kuwa watulivu wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio
hili. Tutawasaka popote walipo na kupambana
nao bila huruma. Aidha, tutakabiliana na
aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna
hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi
yetu. Kamwe hatutakubali kuwaacha
wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa Serikali,
kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa
ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete
anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao
wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia
anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee
na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete vilevile
anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la
kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa
Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia