WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali ina kazi kubwa ya kushughulika na
kundi dogo linalojihusisha na lugha za uchochezi wa kidini ambao
unachangia kudhoofisha amani ya nchi.
“Tunajua
nia yao ni kufanya nchi isitawalike lakini sisi tumesema hatukubali.
Tumekubaliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, ulinzi uimarishwe kila
mahali, mshingae kuona watu wanawahoji lakini nia njema, ya kurudisha
amani yetu,” alisema Waziri Mkuu.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Mei 10, 2013) wakati akiwasilisha salamu
za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati wa ibada ya mazishi ya
waumini watatu wa Kanisa la Mt. Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti,
jijini Arusha waliofariki dunia kutokana na mlipuko wa mabomu uliotokea
Jumapili iliyopita, Mei 5, mwaka huu kanisani hapo.
Waziri
Mkuu amewaomba wanachi kutoka ushirikiano kwa vyombo vya dola kwa kutoa
taarifa zozote zitakazosaidia kwenye upelelezi wa tukio hilo.
“Ninawaomba
Watanzania tushirikiane kuwafichua watu hawa waovu kwa sababu tunaishi
nao, ni watu ambao wako miongoni mwetu... Tusaidieni kutunong’oneza ili
tuchukue hatua, alisema.
Waziri
Mkuu alisema yeye ni miongoni mwa watu wanaoamini kwamba ukristo au
uislamu hauwezi kuondolewa kwa kuwaua viongozi wa dini au waumini wao.
“Ni kujidanganya tu mtu akiamini kuwa akimuua Askofu, Mufti au Muumini
ataimaliza dini yoyote. Madhehebu haya mawili ni nguzo kubwa kwa Taifa
letu, tunatamani tuendelee kuwa na amani iliyokuwepo siku zote,”
alisisistiza.
Alisema Serikali kupitia idara ya maafa itatoa sh. milioni 100/- ili zisaidie kukabiliana na janga lililowakabili wana Arusha.
Mapema,
akiongoza ibada hiyo, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwataka
waumini wote kutolipa uovu kwa uovu bali watende wema ili kusahihisha
maovu. “Ishara ya uovu imetendwa na hawa watu dhidi ya waumini wenzetu
kwa madhumuni yanayojulikana na wao tu bila kuchokozwa na hawa marehemu
ama wale waliko hospitali (majeruhi),” alisema.
“Uovu
umeshatendwa, je sisi tufanye nini? Angekuja hapa kanisani yule
aliyesababisha mauti haya, tungemfanya nini?” Alihoji Kardinali Pengo na
kujibiwa na mamia ya waumini waliohudhuria ibada hiyo: “Tungemsamehe.”
Aliwasihi
waumini wote kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili tukio hilo na
lile la kuuawa kwa Padre Evarist Mushi kule Zanzibar yasiwe sababu ya
kusambaratika kwa amani ya Taifa hili.
“Tusilipe ubaya kwa ubaya, tuendelee kuomba Mungu asikie sala yetu na awazindue wenye mamlaka watimize wajibu wao,” alisema.
Naye
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk.
Alex Malasusa akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Jukwaa la
Wakristo Tanzania (TCF), alilaani waliosababisha mauaji hayo na kusema
kitendo hicho kimelitia doa Taifa kwa vile ni kitendo kinachoashiria
kuchafua amani ya Tanzania.
Aliwasihi
waumini wote kutokuwa waona katika kazi ya kumtanga za Kristo. “Risasi
zinapigwa, mioto inayowashwa katika makanisa yetu na mabomu
yanayolipuliwa yasiwe sababu ya kututia hofu. Imani yetu haiko katika
miili bali iko mioyoni mwetu,” alisema.
Askofu
Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu la Arusha akitoa shukrani kwa niaba
ya Kanisa Katoliki aliwashukuru wote waliofika kuwafariji kutokana na
tukio hilo na kuwathibitishia kuwa kama Kanisa wameguswa na moyo
waliouonyesha.
“Tupige
goti, ndiyo kazi tuliyonayo. Tupige goti ili Mungu awafichue hawa watu,
aufichue mfumo wao wa kiovu, na awape nguvu viongozi wetu wao ni kama
sisi na iko siku watatoa hesabu mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema.
Aliwasihi
waumini wote kutoogopa na kuendelea kuomba ili waliohusika na uovu huo
Mungu awafichue na kuwaonyesha hadharani. “Ninaambiwa msiogope, hakuna
kutishwa kwa namna yoyote tunaposimama na Kristo... sisi hatupaswi
kuogopa kwa sababu Kristo alishinda mauti,” alisisitiza.
Watu
66 waliathirika kutokana na mlipuko huo uliotokea Mei 5, mwaka huu
ambapo watatu wamefariki dunia na kati ya wagonjwa 63 waliobakia, wanane
walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wengine waliotibiwa na
kuruhusiwa kurudi nyumbani, na baadhi wanaendelea kupatiwa matibabu
mjini Arusha.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,