AOMBA LUBANGA AFUNGWE MIAKA 30,MASHITAKA YA GBAGBO SASA KUSIKILIZWA AGOSTI 13
Wakati mwendesha mashitaka wa
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) wiki hii ameomba mahakama
hiyo imhukumu kifungo cha miaka 30 jela kiongozi wa zamani wa
wanamgambo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Thomas Lubanga
baada ya kutiwa hatiani, usikilizaji wa uthibitisho wa mashitaka dhidi
ya Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo umeahirishwa hadi Agosti 13.
ICC
Ataka Lubanga afungwe miaka 30 jela:
Alhamisi,mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai (ICC), Luis Moreno Ocampo aliiomba mahakama hiyo imhukumu kifungo
cha miaka 30 jela kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Thomas Lubanga. Lubanga (51) alitiwa
hatiani na mahakama hiyo Machi 14, mwaka huu kwa uhalifu wa kivita kwa
kuwasajili watoto wa chini ya miaka 15 kupigana vita Mashariki mwa DRC.
Uthibitisho wa mashitaka dhidi ya Gbagbo waahirishwa hadi Agosti 13:
Mahakama ya ICC, Jumatano iliahirisha usikilizaji wa uthibitisho wa
mashitaka dhidi ya Rais wa zamani waIvory Coast, Laurent Gbagbo hadi
Agosti 13. Awali usikilizaji huo ulipangwa Juni 18, lakini wakili wake
aliomba muda zaidi wa kujiandaa.Gbagbo anakabiliwa na mashitaka ya
uhalifu dhidi ya binadamu.
Wapingana tarehe za kuanza kusikilizwa kesi za Wakenya wanne:
Wakati watuhumiwa watatu kati ya wanne katika kesi ya kuhusika katika
ghasia zilizotokea nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007
wanataka kesi yao ianze kusikilizwa Machi mwakani mbele ya ICC, mwenzao
mmoja, Francis Muthaura, Mkuu wa zamani wa Utumishi,aliomba kesi yake
ianze kusikilizwa Septemba, mwaka huu.Watuhumiwa walioomba kupitia kwa
mawakili wao,kesi zao zisikilizwe Machi mwakani ni pamoja na Naibu
Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta na Mbunge William Ruto, wote wawili
wanatarajiwa kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao wa Kenya
unaopangwa kufanyika mwakani.Mwingine aliyeunga mkono muda huo
uliopendekezwa ni Mwandishi wa habari Joshua Sang.
Mwendesha mashitaka mpya wa ICC aapishwa:
Mwendesha Mashitaka mpya wa ICC, Fatou Bensouda, raia waGambia,
anaapishwa leo (Juni 15) kuchukua nafasi ya Luis Moreno Ocampo
waArgentina aliyemaliza muda wake wa kazi baada ya kutumikia mahakama
hiyo kwa miaka tisa.
WIKI IJAYO
Rwanda
Mahakama za Gacaca kufungwa rasmi:
Mahakama za jadi nchiniRwanda maarufu kwa jina la Gacaca, ambazo
zilitumika katika kuendesha na kuhukumu maelfu ya kesi za mauaji ya
kimbari yaRwanda zitafungwa rasmi Jumatatu ijayo.
ICTR
Hukumu ya kesi ya afisa wa mwisho wa jeshi kushitakiwa ICTR Jumanne ijayo:
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne
ijayo itatoa hukumu katika kesi inayomkabili afisa wa zamani wa jeshi
laRwanda, Kapteni Idelphonse Nizeyimana.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia