JAMII YATAKIWA KUTAMBUA UMUHIMU WA KUWALINDA WATOTO
JAMII imetakiwa kutambua umuhimu wa kuwalinda watoto na
kufahamu haki zao za msingi huku wakitambua kuwa swala la kuwalinda watoto ni la kwetu sote badala ya kuwaachia
serikali na mashirika binafsi.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa shirika la Mkombozi la mjini
Arusha, Herry Adili wakati akizungumza katika tamasha lililolenga haki za mtoto na kuwashirikisha wadau mbalimbali
kutoka kwenye jamii juu ya umuhimu wa kumlinda mtoto na kumpatia haki zao za
msingi.
Alisema kuwa, jamii inayowazunguka watoto hao ndio inayopaswa
kuhakikisha inawalinda na matukio mbalimbali ya unyanyasaji yanayofanya kwenye
jamii zao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mtoto anapewa nafasi ya kushiriki
kikamilifu badala ya kunyanyapaliwa.
Alisema kuwa,umefika wakati sasa wa jamii kuchukua hatua na
kuanza kutokomeza matukio mbalimbali ya unyanyasaji wanayofanyiwa watoto hao na kujikuta wengi
wao wakiishia mitaani na hata wengine kujiunga na makundi mbalimbali yanayowapotosha.
Aliongeza kuwa,jamii inapaswa kutambua kuwa ina wajibu mkubwa
sana wa kumlinda mtoto yoyote aliyeko katika jamii kwa kumpatia haki zake za
msingi badala ya kutegemea mashirika mbalimbali na serikali kufanya mambo hayo.
Naye Mwelimishaji
kutoka shirika hilo la Mkombozi ,Fredrick Mbise alisema
kuwa shirika hilo limeweza kufanya utafiti wa awali chini ya ofisa wa shirika hilo raia wa kigeni,Anna Spector kuhusu haki za
watoto na hisia zao juu ya ulinzi,kuanzia mwezi machi hadi mei mwaka
huu,ambapo limebaini kuwa watoto hao wanaelewa haki zao.
Alisema utafiti huo ulieleza kuwa, theluthi mbili ya watoto
wanaamini kwamba wazazi au watu wazima wana uwezo wa kuondoa haki za watoto na
nusu ya watoto walisema kuwa wazazi ndio wanaoamua ni haki zipi ambazo watoto wanapaswa kuwa
nazo.
Alisema kuwa, jumla ya watoto 745 walishiriki katika utafiti
huo ambapo kati ya hao watoto 603 wanatokea mashuleni huku watoto 142 wapo
kwenye jamii , ambapo maeneo yaliyofanyiwa utafiti huo ni moshi mjini ,moshi vijijini na manispaa ya
Arusha .
Aliongeza kuwa, watoto wengi wanahitaji haki zao za msingi
kama vile kupata elimu, mavazi,malazi, chakula na ulinzi na endapo watapatiwa
haki zao itawasaidia kwa kiasi kikubwa
sana kutulia na hatimaye kujidhamini wao wenyewe.
Alisema kuwa, baada ya utafiti huo wamechukua uamuzi wa
kuwajulisha wadau mbalimbali katika jamii juu ya umuhimu wa kumjali mtoto na kumpatia
haki zake za msingi ikiwa ni pamoja na kumlinda juu ya matukio mbalimbali ya
unyanyasaji .
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia