WAKILI MWALE KUREJESHEWA FEDHA NA MAGARI YAKE MAHAKAMA YAAMURU


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Arusha imewaagiza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DPP), Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha kuyarudisha magari saba na simu za mkononi kwa Wakili maarufu mkoani Arusha, Mediam Mwale, anayetuhumiwa kupatikana na fedha chafu.

Akisoma hukumu hiyo katika kesi hiyo ya jinai namba 330/11 wiki iliyopita, Hakimu Mkazi Mfawidhi Charles Magesa, alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote, mahakama imeridhika kuwa mamlaka hizo zilikamata magari hayo kinyume cha sheria ya matunda ya uhalifu (Proceeds Crimes Act) pamoja na vifungu namba 41 na 44 vya sheria ya mwenendo wa kesi za jinai.

“Ukamataji  huo ni kinyume cha sheria kutokana na kitendo cha upande wa mashitaka cha kukamata magari hayo, hivyo mahakama inaamuru kuwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai  nchini, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa TRA nchini na Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha ambao walihusika katika zoezi la ukamataji kuhakikisha wanayarudisha yote kwa mshitakiwa nyumbani kwake walikoyachukua,” alisema hakimu huyo.

Magari ambayo mahakama hiyo iliamuru kurudishwa nyumbani kwa mshitakiwa ni T 690 BEW aina ya Range Rover, T 643 BTS Land Rover Discovery, T 907 BTS BMW, T 118 BRS Cadillac Escalade, T 499 APX Land Cruiser, T 520 BBJ BMW, ambayo yalichukuliwa Novemba mosi pamoja na gari  T 660 BCG Toyota Chaser lililokamatwa Desemba 8, mwaka jana.

Mwale ambaye yupo rumande katika gereza kuu la Mkoa wa Arusha la Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na dhamana, alitoa malalamiko mahakamani hapo Desemba 20 mwaka jana na kumtaja ofisa mmoja wa Polisi, Selemani Nyakulinga, kwamba alifika nyumbani akiwa na wenzake na kuchukua magari hayo bila amri ya mahakama.

Aliieleza mahakama kuwa baada ya magari hayo kuchukuliwa yalipelekwa ofisi ya TRA Mkoa wa Arusha bila kuwapo sababu za kilichopelekea magari hayo kukamatwa, hivyo kuiomba mahakama hiyo kutoa amri ya kuachiwa kwani yalikamatwa kinyume cha kifungu namba 28 cha sheria ya kudhibiti fedha chafu na kifungu namba 24 cha Sheria ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Kufuatia malalamiko hayo, Wakili wa Serikali Neema Ringo, aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo ili aweze kufanya utafiti kuhusiana na malalamiko ya mshitakiwa na zaidi awe katika nafasi nzuri ya kujibu.

Mahakama ilikubali ombi hilo na kesi hiyo ilipangwa kuendelea tena Januari 5 mwaka huu. hata hivyo siku hiyo ilipowadia mawakili wote wa serikali wanaoendesha kesi hiyo hawakutokea mahakamani isipokuwa wakili mmoja tu.

Wakili huyo wa serikali aliitaarifu mahakama hiyo kuwa mawakili hao wameshindwa kufika baada ya kukabiliwa na majukumu mengine, hata hivyo mahakama hiyo haikuridhika na sababu hiyo, hivyo kupanga kutoa uamuzi Januari 19, mwaka huu.

Hata hivyo, Januari 19 Hakimu Magesa anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo na kesi iliahirishwa hadi Januari 31 mwaka huu ambapo pia hakimu huyo hakuwepo na kesi kuahirishwa hadi Februari 22 mwaka huu ambapo upande wa mashitaka ukiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Bibi Mlay ulitoa utetezi wake kwa barua, ambapo uliieleza mahakama kwamba magari hayo hayakuchukuliwa na Polisi bali na maofisa wa TRA kuhusiana na masuala ya kodi.

Alisema kuwa kuwapo kwa maofisa wa polisi wakati wa zoezi hilo kusimfanye mshitakiwa kudhani kuwa ndio waliochukua magari hayo bali walisimamia uchukuaji. Alijitetea kuwa gari namba T 520 BBJ lilikabidhiwa kwa wakili wa mshitakiwa Agosti 18, 2011 na kuhusu simu za mshitakiwa alisema kuwa hazikurejeshwa kwake kwa sababu zilipelekwa kwenye kitengo cha polisi cha uchunguzi.

Hata hivyo Hakimu Magesa katika hukumu yake hiyo aliileza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa aliitaarifa mahakama kwamba alituma ndugu zake TRA kuulizia kuhusu magari yake ambapo ndugu zake walitaarifiwa na maofisa wa TRA kwamba magari hayo yalikamatwa kwa maagizo ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) E.S.A. Mmari, kwa barua yake ya Desemba 15, mwaka jana na ndugu wa mshitakiwa walipatiwa nakala ya barua hiyo.

Aliongeza kuwa ni muhimu kuelewa awali kabla kwamba mshitakiwa bado ni mtuhumiwa tu na mtu asiye na hatia hadi hapo itakapothibitishwa vinginevyo na upande wa mashitaka, hivyo anapaswa kutendewa kama mshitakiwa na si kama mtu aliyetiwa hatiani.

“Hoja kubwa ni kwamba magari yake pamoja na ya marafiki zake yamekamatwa na kuchukuliwa bila kuzingatia sheria, na makosa ambayo mshitakiwa ameshitakiwa nayo yapo chini ya sheria ya udhibiti wa fedha chafu ya 2006 na kifungu namba 28 cha sheria hiyo kinaeleza kwamba utaratibu wa kukamata, ukusanyaji taarifa, utaifishaji au ukamataji na udhibiti wa mali utakuwa kama ulivyo chini ya sheria ya matunda ya uhalifu (Proceeds Crimes Act & The Criminal Procedure Act 1991).

“Sheria hiyo ya matunda ya uhalifu ya mwaka 1991 inatoa utaratibu wa namna ya mali ya mtu aliyotiwa hatiani au aliyeshitakiwa na makosa yanayohusiana na sheria hiyo itakavyokamatwa…kifungu muhimu katika sheria hiyo ni kifungu namba 31 (1)” aliieleza mahakama.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post