Katika
kikao cha Bunge la Bajeti kinachoendelea hivi sasa mjini Dodoma, Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe alilazimika
kusimama na kutoa majibu kwa swali lililoulizwa na Mbunge wa Konde,
Khatibu Said Haji (CUF) aliyetaka kujua msimamo wa Tanzania kuhusu suala
la kuridhia ndoa za watu wa jinsia moja hasa baada ya shinikizo la nchi
wahisani kuwa awtasitisha misaada kwa nchi zitakazoweka vikwazo kwa
watu wa kundi hilo.
Akijibu
swali hilo Membe ameelezea msimamo wa Tanzania, Membe amesema sheria ya
ndoa ya mwaka 1971 inatafsiri ndoa kuwa ni muungano wa hiari kati ya
mwanamume na mwanamke wenye lengo la kudumu katika maisha ya wawili hao.
Akasema
suala la msingi ni kuwa, kulingana na matakwa ya sheria ya Tanzania ili
kuwepo na ndoa inayotambulika kisheria ni lazima kuwepo na pande mbili
za jinsia tofauti, yaani mwanamume na mwanamke.
“Dini
zetu zote za hapa nchini hazikubaliani na uwepo wa ndoa za jinsia moja
na viongozi wake wapo kwenye mstari wa mbele kukemea jambo hili,”
alisema Membe.
Akasema
utamaduni wetu na sheria zetu hazitambui ndoa ya jinsia moja. Akasema
muungano kati ya watu wa jinsia moja, yaani mwanamume na mwanamume
mwingine au mwanamke na mwanamke mwingine hautambuliki kama ndoa
kisheria nchini Tanzania.
Katika
swali la nyongeza, Haji pia alitaka kujua ni mikakati gani Tanzania
imejiwekea endapo nchi hizo wahisani zitasitisha misaada yao kwa nchi
hii, kutokana na msimamo wake ambapo Membe alisema fursa za kiuchumi
ambazo zimeendelea kuibuliwa nchini ni moja ya mikakati ya Serikali
kuhakikisha kuwa inajitegemea kiuchumi badala ya kuzitegemea nchi
wahisani.
Alitoa
mfano wa gesi iliyovumbuliwa katika mikoa ya Kusini kuwa ni moja ya
nguzo ya uchumi ambayo Tanzania itaitumia ili iweze kujiendesha kiuchumi
mara nchi wahisani waking’ang’ania sharti hilo la kuruhusu ushoga.
Membe akasema rasilimali hizo na nyingine zikitumiwa vizuri hakuna taifa
ambalo litaichezea Tanzania ovyo ovyo kwa kuwapa masharti ya ajabu.
Membe
amesema itakapotokea wahisani wanasitisha misaada kwa sababu ya msimamo
wa Tanzania wa kupinga ndoa za jinsia moja, Watanzania wako tayari
kujifunga mikanda na kujibeba wenyewe badala ya kukubali kudhalilishwa
utu na utamaduni wao.
Membe
ameliambia Bunge kuwa Tanzania itaendelea kupokea misaada ile tu ambayo
haina masharti ya kubadili sera, utamaduni na sheria za nchi kuhusu
ndoa za jinsia moja.
“Nchi
marafiki duniani zikiwemo zile za Magharibi, zimeendelea kutuheshimu
kutokana na msimamo wetu huo thabiti na usiotetereka kwa kuendelea kutoa
misaada ya ushirikiano wa kiuchumi kwa Serikali ya Tanzania,” alisema
Membe