MAHAKAMA ya hakimu mkazi Arusha, imemwagiza Meneja wa
mamlaka ya mapato (TRA)mkoani Arusha ,kutekeleza amri ya mahakama kwa kukabidhi
haraka magari saba ya kifahari ya wakili maarufu nchini Median Mwale
inayoyashikilia.
Akitoa maamuzi hayo hakimu
mfawidhi wa mahakama hiyo,Charles Magesa alisema kuwa kitendo cha mawakili wa
serikali Fredrick Manyanda na Neema Ringo kuendelea kuzuia magari hayo ambayo
mahakama ilishayatolea maamuzi ni kuidharau mahakama na ni kinyume cha sheria .
Alisema kuwa tangu kufunguliwa kwa shauri hilo la jinai lililofunguliwa agosti 9 mwaka jana,linalomkabili mshitakiwa Mwale, shauri
hilo limeshindwa kuendelea kutokana na mawakili wa serikali kuendelea kuweka
mapingamizi yasiyo ya msingi ya kuzuia magari ya mshitakiwa Mwalena kusababisha
kutoendelea kwa kesi ya msingi inayomkabili.
Hakimu Magesa alisisitiza
kuwa kitendo cha mawakili wa serikali kupitia ofisi ya mwanasheria mkuu,
kuandika barua TRA ya kuzuia maamuzi ya
mahakama ya kuitaka TRA mkoani hapa isikabidhi magari hayo ni utovu wa nidhamu
na ni kinyume cha sheria ,kwani alisema
hakuna mwenye mamlaka ya kuzuia amri halali ya mahakama ispokuwa mahakama za
juu pekee .
Hakimu huyo alisema awali mahakama
hiyo ilitoa hukumu Machi 7 mwaka huu yakutaka wakili Mwale arudishiwe
magari hayo hata hivyo upande wa serikali haukuridhika na maamuzi hayo na
kukata rufaa mahakama kuu chini ya Jaji Kakusulo Sambu.
Alisema kuwa, mahakama
hiyo iliridhika na maamuzi ya hakimu Magesa na kutaka faili la kesi hiyo
lirudishwe katika mahakama hiyo ya
hakimu mkazi kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa shauri la msingi linalomkabili.
Hata
hivyo mawakili hao wa serikali waliendelea kupiga danadana na mara nyingi wamekuwa
hawafiki mahakamani na wakifika wanatoa sababu zisizo kuwa za msingi na kufanya
kuahirishwa kwa shauri hilo.
Wakati huo huo;hakimu
Magesa ametupitia mbali maombi ya mawakili wa serikali waliyowasilisha
mahakamani hapo ya kutaka ajitoe kwenye shauri hilo ili haki iweze kutendeka
wakidai kuwa ,hakimu Magesa amekuwa na ukaribu na ndugu wa mshtakiwa.
Pia alidai kuwa mawakili
hao walitoa sababu nyingine kuwa ofisi ya mshitakiwa Mwale ipo jijini Arusha
huku mahakama nayo ikiwa Arusha hivyo kutakuwa na
mwingiliano kiutendaji na kufanya haki
isitendeke,kadhalika sababu nyingine
wakidai mshitakiwa ni mkazi wa Arusha
hivyo anaweza kuwa na mwingiliano naye wa karibu ama ndugu zake.
Hakimu Magesa alisema baada
ya kuzipitia hoja hizo alibaini kuwa hazina mashiko na wala haziihitaji elimu
ya darasa la saba kuzielewa na kuwataka mawakili hao kurudi darasani ili
kujiridhisha na elimu walio nayo ,kwani ameshangazwa na mawakili hao wasomi
tena wa ngazi za juu kuwa mbumbumbu wa
kutojua vifungu vya sheria kwa kutoa hoja zisizo za msingi kama hizo.
Alisisitiza kuwa mahakama
haitoi maamuzi yanayowapendeza wao bali inafuata sheria katika kutekeleza
maamuzi yake ili haki iweze kutendeka ,hata hivyo alifafanua kuwa sababu za msingi za kutaka hakimu ajitoe
ni pamoja na ushahidi unaoonyesha kuwa hakimu ama jaji ana mahusiano ya kindugu
yenye maslahi na wahusika wa kesi.
Aidha alisema sababu nyingine
ni kuwepo kwa ushahidi unaoonyesha kuwepo kwa manufaa kwa jaji ama hakimu kwa mshtakiwa katika shauri la kesi husika.
Alisema kutokana na sababu
hizo upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha hoja zao ,hivyo hakimu Magesa
alisema mawakili hao wanajaribu kupoteza muda katika shauri hilo na kuutaka upande wa
mashtaka kukamilisha upepepezi haraka ili kesi ya msingi iweze kumalizika na
sio kupoteza muda kwa sababu zisizofaa.
Hata hivyo hakimu magesa
aliwataka mawakili hao wa serikali kuacha kuchezea kodi za wananchi katika kesi
hiyo kwa kutumia gharama kubwa kusafiri,kula
na kulala hotelini kwa kuwa wamekuwa wakichelewesha kesi hiyo kwa
kuahirishwa huku wakiiambia mahakama kuwa maofisa wao wako nje ya nchi
wakifuatilia nyaraka mbalimbali za kesi hiyo.
Hakimu Magesa aliahirisha
shauri hilo hadi julai kumi na tatu mwaka huu litakapotajwa tena na kuwataka
mawakili wa serikali kufika mahakamani hapo.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia