VIFO VYA WACHIMBAJI MERERANI VYA SABABISHWA NA UZEMBE

 vifo vinavyotokea kwenye machimbo ya madini ya
Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara
vinatokana na uzembe katika uchimbaji wa baadhi ya migodi hiyo.

Hayo yameelezwa  na Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini
Mhandisi Benjamin Mchwampaka kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo
mameneja wa migodi yaliyofanyika ukumbi wa Kazamoyo Inn mjini
Mirerani.

Mhandisi Mchwampaka alisema kuwa tangu mwezi Januari hadi Mei mwaka
huu wachimbaji wadogo 11 wamepoteza maisha kwenye machimbo ya migodi
ya Tanzanite katika matukio tofauti.



Pia alikemea vikali tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo kutumia
baruti kama silaha badala ya kuzitumia kwa nyenzo za kazi kwa
kuzifanya mabomu ya kienyeji na kuwalipua wachimbaji wenye migodi
yenye uzalishaji.

“Serikali haitavumilia tena vitendo hivi na wote watakaohusika na
jambo hilo mgodi wao utafungwa mara moja na tutafuta leseni zao kabla
ya kuwachukulia hatua nyingine za kisheria,” alisema Mchwampaka.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Chama cha wachimbaji madini mkoa wa
Manyara (Marema) Zephania Mungaya aliishukuru Serikali kutoa mafunzo
hayo ambayo yatawanufaisha wachimbaji wadogo kupitia mameneja hao wa
migodi.

“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali kwa kuandaa
mafunzo haya ambayo yatazidi kuwajengea uwezo mameneja wa migodi ambao
ndiyo daraja baina ya wamiliki wa migodi,wachimbaji na Serikali,”
alisema Mughaya.

Naye,Ofisa madini mkazi wa Mirerani Laurent Mayala alisema lengo la
mafunzo hayo ni kupunguza ajali migodini kwa kuwaongezea mbinu na
elimu ya usalama na sheria ya madini ili kuboresha hali ya uchimbaji
salama migodini.

Mayala alisema mada zitakazotolewa ni usalama migodini,uzoefu na
changamoto,sera na sheria ya madini,upelekwaji hewa migodini,matumizi
ya baruti na tahadhari zake,wajibu na majukumu ya meneja na jiolojia
ya miamba ya Tanzanite.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia