Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumatano
imekubali maombi ya mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo ya kuhamishia
kesi ya mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambaye bado anasakwa, Charles
Ryandikayo,kwenda kusikilizwa nchini Rwanda, ikiwa kesi ya sita
kuhamishiwa nchini humo.
Mahakama
iliyotoa maamuzi hayo ikiongozwa na Jaji, Vagn Joensen imeeleza kwamba,
kwa kuzingatia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili, imefikia
uamuzi wa kuhamishia kesi hiyo nchini Rwanda.
‘’Mahakma
imeamua kesi kupelekwa kwenye mamlaka ya Jamhuri ya Rwanda ili wenye
mamlaka hayo kuiwasilisha kesi hiyo mbele ya Mahakama Kuu ya Rwanda kwa
ajili ya kuanza kusikilizwa kwa haraka,’’ inasomeka sehemu ya uamuzi
huo.
Imeelezea
matumaini yake kwamba’’Jamhuri ya Rwanda, kwa kukubali kupokea kesi
kutoka mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa, itatimiza wajibu wake kwa
uaminifu, uwezo na nia njema ya kuendesha kesi hiyo kwa kufuata viwango
vya juu vya haki vya kimataiafa.’’
Ryandikayo
ambaye alikuwa Meneja wa mgahawa mmoja wa Mubuga katika wilaya ya
Gishyita mkoani Kibuye, Magharibi ya Rwanda anashitakiwa kwa mauaji ya
kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo, uhalifu dhidi ya binadamu na
uhalifu wa kivita.ICTR imeshatoa maamuzi katika maombi matano kama
hayo.
Maombi
hayo yanahusu mtu mwingine ambayo bado anasakwa pia, Ladislas
Ntaganzwa, meya wa zamani wa wilaya ya Nyakizu, mkoani Butare, Kusini
mwa Rwanda na Bernard Munyagishari, anayedaiwa kuwa kiongozi wa
wanamgambo wa Interahamwe mkoa wa Gisenyi, Kaskazini ya Rwanda.Lakini
upande wa utetezi unatarajiwa kupinga maamuzi hayo.
Maombi
mengine matatu ya aina hiyo ambayo yameshatolewa uamuzi na ICTR
yanawahusu, Mchungaji Jean Uwinkindi na watuhumiwa wawili ambao nao bado
wanasakwa ikiwa ni pamoja na Fulgence Kayishema na Charles Sikubwabo.
Maombi
mengine mawili ya aina hiyo ambayo yapo mbele ya mahakama yakisubiri
uamuzi ni pamoja na ya Aloys Ndimbati, meya wa zamani wa Gisovu na
Luteni Kanali Pheneas Munyagishari, kamanda wa zamani wa kambi ya jeshi
ya Gako, wilayani Kanzenze katika mkoa wa Kigali Vijijini.