MAHAKAMA ZA GACACA ZAFUNGWA, NIZEYIMANA KUTUMIKIA KIFUNGO CHA MAISHA

Wakati  Rais Paul Kagame wa Rwanda wiki hii alifunga rasmi mahakama za jadi za Gacaca zilizotumika kuendesha kesi za mamilioni ya watuhumwia wa mauaji ya kimbari, Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji hayo, (ICTR) imemhukumu kifungo cha maisha jela afisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo, Idelphonse Nizeyimana baada ya kutiwa hatiani kwa kuhusika kwake katika mauaji hayo.
RWANDA
Kagame afunga rasmi mahakama za Gacaca: Rais Paul Kagame wa Rwanda Jumatatu wiki hii alifunga rasmi mahakama za jadi za Gacaca zilizotumika kuendesha kesi za mamilioni ya watuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.
Alisema mahakama za gacaca zimedhihirisha uwezo wa Rwanda wa kuweza kujitafutia suluhisho wenyewe kwa matatizo yao na watu wake kufanya maamuzi juu ya mambo yanayohusu maisha yao. Mahakama hizo zilianza kazi mwaka 2002.

ICTR

Nizeyimana ahukumiwa kifungo cha maisha jela: Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne imemhukumu kifungo cha maisha jela afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kapteni Idelphonse Nizeyimana baada
ya kumtia hatiani kwa kuhusika kwake kwa mauaji ya kimbari akiwemo Malkia wa mwisho waRwanda, Rosalie Gicanda. Alitiwa hatiani kwa kuamuru mauaji ya kimbari, kuteketeza kizazi na mauaji kama ukatili dhidi ya binadamu katika maeneo mbalimbali mkoani Butare, Kusini mwa Rwanda Aprili, 1994.Upande wa utetezi unakusidia kukata rufaa.

Kesi ya Ryandikayao kusikilizwa nchini Rwanda: ICTR Jumatano wiki hii pia imekubali maombi ya mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo ya kuhamishia kesi ya mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambaye bado anasakwa, Charles.
Ryandikayo,kwenda kusikilizwa nchini Rwanda, ikiwa kesi ya sita kuhamishiwa nchini humo. Ryandikayo ambaye alikuwa Meneja wa mgahawa mmoja wa Mubuga katika wilaya ya Gishyita mkoani Kibuye, Magharibi ya Rwanda anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.
Madai ya Zigiranyirazo kulipwa fidia yakataliwa: ICTR wiki hii pia imeyatupa maombi ya Protais Zigiranyirazo aliyeachiwa huru na mahakama hiyo kutaka alipwe fidia ya dola milioni moja kwa madai ya kukiukwa kwa haki zake za msingi.Zigiranyirazo, maarufu kwa jina la Mr. Z ambaye ni shemeji wa Rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, alikataliwa pia ombi lake jingine la la kutaka mahakama kuiamuru Ubelgiji kutoa ushirikiano wa kumruhusu kurejea katika nchi hiyo alikokamatwa hapo mwanzo ili kuungana na familia yake.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post