Mahakama
ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne imemhukumu
kifungo cha maisha jela afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kapteni
Idelphonse Nizeyimana baada ya kumtia hatiani kwa kuhusika kwake kwa
mauaji ya kimbari ya akiwemo Malkia wa mwisho wa Rwanda, Rosalie
Gicanda.
Jaji
Lee Muthoga aliyekuwa anaongoza jopo la majaji watatu, alitamka adhabu
hiyo baada ya kumtia hatiani afisa huyo kwa kuamuru mauaji ya kimbari,
kuteketeza kizazi na mauaji kama ukatili dhidi ya binadamu katika maeneo
mbalimbali mkoani Butare, Kusini mwa Rwanda Aprili, 1994.
‘’Nizeyimana anahusika katika uhalifu wote huo kupitia ushiriki wake katika kundi la uhalifu,’’ alisema Jaji Muthoga.
Wengine
waliouawa nje ya Malkia Rosalie ni pamoja na maelfu ya wakimbizi
waliokuwa wanapata hifahdi ya maisha yao katika parokia ya Cyahinda na
Profesa mmoja wa Chuo Kikuu cha Rwanda, Pierre Claver Karenzi.
Majaji
katika hukumu hiyo walikataa utetezi wa Kapteni Nizeyimana kwamba kati
ya Aprili 20 na 22, mwaka 1994 na baadaye Aprili 26 hadi mwishoni mwa
Mei, 1994 hakuwepo mkoani Butare.
‘’Utetezi huo hauaminiki na haupingani na ushiriki wa Nizeyimana katika mauaji ya kimbari,’’ majaji walieleza.
Baada
ya hukumu hiyo, John Philpot, Wakili Kiongozi wa Nizeyimana alisema
atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo akidai kwamba ‘’ mahakama
haikufuatilia kwa makini ushahidi ambao kwa kiasi kikubwa umetolewa na
watu waliopangwa maalum kwa kazi hiyo kutoka nchini Rwanda.’’
Aliendelea
kueleza kwamba ‘’mteja wetu alikuwa mpiganaji mzuri, askari mzuri
aliyekuwa anaitetea nchi yake dhidi ya uvamizi na hakuwapo wakati mwingi
yalipokuwa yanatokea matukio haya.’’
Mwendesha
mashitaka pamoja na mambo mengine anadai kwamba mshitakiwa alikuwa mtu
wa pili kimadaraka aliyekuwa anashughulikia Usalama na Operesheni za
Kijeshi katika Chuo cha Maafisa wa Jeshi Wasiokuwa na Kamisheni (ESO),
mkoani Butare.
Nizeyimana
alitiwa mbaroni nchini Uganda, Oktoba 5, 2009 na kuhamishiwa katika
gereza la Mahakama ya Umoja wa Mataifa Arusha, Tanzania, siku
iliyofuata.
Kesi yake ilianza kusikilizwa Januari 17, 2011 na kuhitimishwa Septemba 21, 2011.