KESI
ya wakili maarufu nchini, Median Mwalle, imechukua sura mpya baada ya
wakili huyo kuibua madai mazito mahakamani kuwa mmoja wa watu wake wa
karibu, John Kabwe, alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha siku
chache baada ya kumpa taarifa muhimu.
Mbele
ya Hakimu Mfawidhi, Charles Magesa, anayesikiliza shauri la jinai namba
330/11, Mwalle alisema mtu huyo alikufa mara tu baada ya kuwa
amemweleza mambo fulani muhimu na mazito kwa ajili ya kesi yake.
Hata
hivyo hakueleza kwa kina kifo cha Kabwe kilitokea lini lakini alisema
kuwa siku chache kabla ya kifo chake alikwenda kuzungumza naye na
alimweleza mambo muhimu ambapo alishitushwa baada ya siku chache kupata
taarifa kuwa amefariki dunia.
Taarifa
ya wakili huyo ambayo iliwashitua watu wengi waliofika mahakamani hapo
jana, aliongeza kuwa kifo hicho kimetokea huku kukiwa na vitisho vya
kuuawa kwake na wale wanaomsaidia katika kesi hiyo.
Alibainisha kuwa hata baadhi ya wafanyakazi wake wamekuwa wakikamatwa ovyo na polisi na kuswekwa ndani bila sababu za msingi.
“Mheshimiwa,
mfanyakazi wa kampuni yangu, Said (Kivuyo) alikamatwa akawekwa rumande
kwenye kituo cha polisi siku moja, kosa lake ni kuwaandikia barua
akiwataka warejeshe magari yangu ambayo waliyachukua kinyume cha sheria
pamoja na simu zangu za kiganjani kama mahakama yako ilivyoamua.”
“Kijana
wangu mwingine, Mruma (Yusuph) ambaye huniletea chakula magereza naye
alikamatwa na kuwekwa rumande Kituo cha Kati cha Polisi siku tano,”
wakili huyo alilalamika mahakamani hapo.
Aliwataja
wanaotishia maisha yake kuwa ni pamoja na mawakili wa serikali, Neema
Ringo , Fredrick Manyanda, polisi waliopeleleza shauri lake; warakibu
wsaidizi wa Polisi (ASP) Seleman Nyakulinga na fadhili Mndeme pamoja na
Ofisa Usalama wa Taifa aliyemtaja kwa jina moja la Canute.
Alisema
kuwa anapata wasiwasi huo kutokana na ukweli kuwa watu wote hao kwa
pamoja humfuata mahabusu kwenye Gereza la Mkoa la Kisongo akitaka
kumchukua kwa hati maalumu (removal Order) wakitaka wampeleke kituo cha
polisi kwa mahojiano ambapo huwa anakataa lakini anashangaa kuwa akija
mahakamani siku ya kesi huwa hawatoi maombi hayo ya kutaka kumhoji.
“Mheshimiwa
hakimu naiomba mahakama yako tukufu iweke kumbukumbu maisha yangu yako
hatarini. Wanakuja gerezani wanaomba wanichukue wakanihoji kwa siku tatu
au masaa mawili. Tena wanawalaumu maafisa wa magereza kuwa kwa nini
hawanitesi, kwa kuwa wanaona afya yangu haijabadilika,” alilalama wakili
huyo.
Mwalle
alisema kuwa kinachofanywa na maofisa hao wa serikali haamini kama ni
maelekezo ya serikali bali wanayafanya kwa kusukumwa na utashi wao
binafsi baada ya kubaini masuala wanayomtuhumu nayo na kumshitaki hayana
ukweli hivyo wanadhani akitoka ataifungulia kesi serikali jambo
alilosema hafikirii kufanya.
“Mimi
siwezi kuishitaki serikali yangu ambayo imenisomesha mpaka nikawa
wakili, ninachokiona mheshimiwa hakimu ni kuwa hawa kina Nyakulinga
wanataka wanichukue kwa kuwa wanajua nina presha wanaweza kunifanyia
jambo lolote ili presha yangu ipande nife,” alilalamika wakili Mwalle.
Aidha,
alilalamikia taarifa za uongo zinazoenezwa kuwa alipokamatwa alikuwa
na sh milioni 20 alizodai kuwa ni za matumizi madogo na kwenye akaunti
yake alikutwa na fedha chafu shilingi bilioni 28 na akaunti nyingine
shilingi bilioni 19 huku wakimhusisha na kundi la kigaidi la Al Shabab,
jambo alilosema kuwa si kweli kwani katika kesi zilizopo mahakamani hapo
hakuna hata moja inayohusiana na mambo hayo.
Kwa
upande wake wakili wa serikali, Timon Vitalis, alimtoa wasiwasi Wakili
Mwalle kwa kumweleza kuwa hawawezi kumuua kutokana na ukweli kuwa
wakimchukua gerezani taarifa zitaonyesha amechukuliwa na nani na muda
gani.
Hata
hivyo alisema kuwa suala hilo ataliwasilisha kwenye ofisi zao ili
kuwezesha haki kutendeka na Mwalle aione kutendeka ambapo alisema kama
itabidi itaundwa tume ya kuchunguza suala hilo.
Hakimu
Magesa alisema kwa kuwa jalada la kesi hiyo liko Mahakama Kuu kwa ajili
ya kufanyiwa mapitio baada ya upande wa serikali kutoridhika na uamuzi
wa kutakiwa kurejesha magari ya Mwalle, aliahirisha shauri hilo mpaka
Aprili 11, mwaka huu siku ambayo Mahakama Kuu itakuwa inapitia maamuzi
hayo ambapo wakimaliza ndipo litarejea kwake.
Alisema
kuwa anaamini magereza wanajua utaratibu wa kuingia na kutoka mahabusu
ingawa alimtaka wakili wa serikali Vitalis kupeleka malalamiko hayo
kwenye ofisi zao ili yaweze kushughulikiwa.
Mawakili
hao wa serikali wamekata rufaa Mahakama Kuu wakitaka ipitie maamuzi
yaliyofanywa na mahakama hiyo yakiwaagiza Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
nchini (DPP), Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na
Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha kuyarudisha magari saba na simu za mkononi
kwa wakili huyo anayetuhumiwa kupatikana na fedha chafu.
Uamuzi
huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Magesa, ambaye alisema baada
ya kupitia ushahidi wa pande zote, mahakama yake imeridhika kuwa mamlaka
hizo zilikamata magari hayo kinyume cha sheria ya matunda ya uhalifu
(Proceeds Crimes Act) pamoja na vifungu namba 41 na 44 vya sheria ya
mwenendo wa kesi za jinai.
Magari
yaliyoamriwa na mahakama kurejeshwa kwa Mwale ni T 690 BEW aina ya
Range Rover, T 643 BTS Land Rover Discovery, T 907 BTS BMW, T 118 BRS
Cadillac Escalade, T 499 APX Land Cruiser, T 520 BBJ BMW, ambayo
yalichukuliwa Novemba mosi, pamoja na gari T 660 BCG Toyota Chaser
lililokamatwa Desemba 8, mwaka jana.