GATETE APUNGUZIWA KIFUNGO CHA MAISHA, WATU 11 KUWANIA NAFASI YA MSAJILI ICC
Wakati Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne imempunguzia adhabu ya kifungo cha maisha jela afisa mwandamizi wa zamani wa serikali ya Rwanda, Jean-Baptiste Gatete,Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) siku hiyo pia alitangaza majina ya watu 11 watakaogombea nafasi ya Msajili wa Mahakama hiyo.
ICTR
Mawaziri wawili wa zamani waomba kuachiwa huru: Mawaziri wawili wa zamani wa Rwanda, Justin Mugenzi na Prosper Mugiraneza, Jumatatu wiki hii waliiomba Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataiafa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) kubadilishiwa hukumu na adhabu ya miaka 30 jela waliyopewa Septemba 30, 2011.Walitiwa hatiani kwa kula njama za kufanya mauaji na uchochezi.
Gatete apunguziwa adhabu ya kifungo cha maisha: Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne imempunguzia adhabu ya kifungo cha maisha jela hadi miaka 40,afisa mwandamizi wa zamani wa serikali ya Rwanda, Jean-Baptiste Gatete kwa kuhusika kwake na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini mwake. Kupunguziwa adhabu pamoja na mambo mengine kumetokana pia na mahakama ya awali kukiuka haki ya Gatete ya kusikilizwa kwa kesi yake bila kucheleweshwa.Alitiwa hatiani kwa makosa ya mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu.
ICC
Watu 11 kuwania nafasi ya Msajili wa ICC: Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Jaji Sang-Hyun Song amewasilisha majina ya watu 11 wanaowania kuchaguliwa kushika nafasi ya Msajili wa mahakama hiyo, yakiwemo majina mawili kutoka barani Afrika. Majina hayo yamewasilishwa mbele ya Rais wa Baraza Kuu la Wanachama wa Mahakama hiyo Oktoba 9, 2012.
Majaji wasikiliza maombi ya Libya juu ya kesi ya mtoto wa Gaddafi: Mawakili wa Libya Jumanne wiki hii wamesimama mbele ya mahakama ya ICC kutetea maombi yao ya kutaka kesi ya Saif al-Islam anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu isikilizwe nchini Libya, huku wakiahidi kuwa haki itatendeka kwa kesi hiyo. Wamedai, waendesha mashitaka wa Libya wamekusanya ushahidi wa kutosha kumshitaki mtoto huyo wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya, marehemu Muammar Gaddafi. Nao mawakili wa utetezi wamedai kwamba hadhi ya mahakama hiyo itadhurika iwapo kesi hiyo itasikilizwa nchini Libya, ambako wamedai hakuna mashaka kwamba Al-Islam atanyongwa iwapo atapatikana na hatia.
Mahakama Maalum ya Sierra Leone kufungwa mwakani: Rais wa Mahakama ya Maalum ya Sierra Leone, Jaji Sireen Avis Fisher Jumanne aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Mahakama yake ina mpango wa kuhitimisha kazi zake ifikapo mwakani. Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2002 kuwashitaki watu waliohusika katika ghasia na mauaji wakati wa miaka 10 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone. Rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor ameshatiwa hatiani na mahakama hiyo kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu kwa kusaidia na kuunga mkono vita hivyo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 50 jela. Pande zote mbili za mashitaka na utetezi zimekata rufaa kupinga hukumu hiyo.Inakadiriwa kwamba uamuzi wa rufaa hiyo utatolewa Septemba, 2013.
WIKI IJAYO
Kesi ya Bemba kuendelea kusikilizwa wiki ijayo: Kesi ya utetezi inayomhusu kiongozi wa zamani wa kundi la waasi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (MLC), Jean Pierre Bemba inatarajiwa kuendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo Oktoba 15, mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).Bemba anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia