APUNGUZIWA ADHABU TOKA KIFUNGO CHA MAISHA HADI MIAKA 40 JELA





Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne imempunguzia adhabu ya kifungo cha maisha jela hadi miaka 40,afisa mwandamizi wa zamani wa serikali ya Rwanda, Jean-Baptiste Gatete kwa kuhusika kwake na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini mwake. Mahakama imethibitisha kutiwa hatiani kwa Gatete kwa makosa ya mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu. Mahakama ya awali ilimpatia adhabu ya kifungo cha maisha jela, Machi 29, 2011 lakini Mahakama ya Rufaa imempunguzia adhabu baada ya kukubali baadhi ya hoja zake za kukata rufaa.Wakati wa mauaji ya kimbari Gatete alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Wanawake na Masuala ya Watoto. ‘’Mahakama ya Rufaa inabadili adhabu ya kifungo cha maisha jela alichopewa Jean-Baptiste Gatete na kumpatia adhabu ya kifungo cha miaka 40 jela, ambayo pia itazingatia muda aliokwishatumikia tangu atiwe kizuizini Septemba 11, 2002,’’ Jaji Kiongozi Liu Daqun alitamka. Gatete aliyevaa mahakamani suti rangi ya maziwa alionekana akiwa ametulia wakati hukumu hiyo ilipokuwa inasomwa mbele ya ukumbi wa mahakama uliofurika wasikilizaji. Kupunguziwa adhabu kutoka kifungo cha maisha hadi miaka 40 jela kumetokana pia na mahakama ya awali kukiuka haki ya Gatete ya kusikilizwa kwa kesi yake bila kucheleweshwa pasipo sababu za msingi. Alitiwa mbaroni Septemba 11, 2002 nchini Congo-Brazzaville lakini kesi yake ilianza kusikilizwa Oktoba 20,2009,ikiwa ni miaka saba baadaye. Katika mahakama ya awali, Gatete ilionekana na hatia pasipo mashaka yoyote kwa kuhusika na vifo vya mamia au hata maelfu ya Watutsi katika maeneo matatu yalikofanyikia mauaji hayo, Mashariki mwa Rwanda kati ya Aprili 7 na 12, 1994. Maeneo yalikotokea umwagaji damu mkubwa ni pamoja na yale ya kata ya Rwankuba na parokia ya Kiziguro kwenye wilaya ya Murambi katika mkoa wa Byumba na maeneo ya parokia ya Mukarange katika wilaya ya Kayonza, mkoa wa Kibungo. Gatete (59) alitiwa mbaroni nchini Congo-Brazzaville Septemba 11, 2002 na kisha kuhamishiwa makao makuu ya ICTR, Arusha nchini Tanzania.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia