ZAIDI YA MILIONI TANO ZAPATIKANA KWENYE HARAMBEE YA NYUMBA YA KUISHI ASKAI POLISI MANYARA



MKUU wa Mkoa wa Manyara,Elaston Mbwilo ameongoza harambe na kupatikana shilingi 5,050,000 (milioni tano na elfu hamsini) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi askari wa kituo cha polisi cha kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro.

Mbwilo ambaye alichangia shilingi milioni moja alianzisha harambee hiyo ili nyumba hizo za askari wa kituo hicho kipya cha Polisi kata ya Naisinyai zijengwe na waweze kuishi kwani zitawapunguzia askari hao kero ya makazi.

Aliagiza wananchi,viongozi wa kijij na kata ya Naisinyai wakishirikiana na kampuni ya TanzaniteOne kuhakikisha kuwa wanamaliza ujenzi wa nyumba hizo kabla ya mwezi Desemba ili aweze kuzindua rami kituo hicho.

“Nikizindua leo kituo hiki bila kuwa na nyumba za kuishi askari wetu hata ninyi mtanishitaki hivyo nawachangia sh milioni moja na muongeze nguvu mkishirikana na TanzaniteOne ili mjenge nyumba hizo nije nizindue,” alisema Mbwilo.

Kwa upande wake,Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya TanzaniteOne Dotto Medard alisema kituo hicho kimejengwa na wananchi hadi kwenye lenta nao wakamaliza kwa kupaua kuweka umeme,maji na kununua samani za ofisi.

Medard alisema awali kituo hicho kiliwekwa jiwe la msingi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema na hadi kukamilika kwake kampuni ya TanzaniteOne imetumia gharama ya shilingi milioni 60 kukimalizia.

Naye,Diwani wa kata ya Naisinyai,Kilempu Kinoka ambaye alichangia shilingi laki tano kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo za askari polisi wa kituo hicho alimuhakikishia mkuu huyo wa wilaya kuwa watajenga nyumba hizo.

“Kwa nafasi ya pekee mkuu wa mkoa hili tutalitekeleza kwani kata ya Naisinyai inaongoza hapa nchini kwa ulinzi shirikishi na polisi jamii kwa hiyo hili litafanyika kwa juhudi kubwa na moyo thabiti,” alisema Kinoka.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya TanzaniteOne,Weseel Marias alisema kampuni yake na jamii ya eneo hilo watajipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa agizo hilo la mkuu wa mkoa linatekelezwa ili azindue kituo cha polisi na nyumba za askari.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia