WAZAZI WATAKIWA KUWAJALI WATOTO WAO

Diwani wa Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,Lucas Zacharia akimkabidhi cheti cha kuhitimu kidato cha nne mwanafunzi wa shule ya sekondari Naisinyai,Roda Yonah kwenye mahafali ya nne ya shule hiyo 
JAMII Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara imetakiwa kuwajali watoto wao kwa kujenga mabweni kwani baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Naisinyai kila siku hutembea kilomita 20 kwenda shule na kurudi nyumbani.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Lucas Zacharia kwenye mahafali ya nne ya shule ya sekondari Naisinyai iliyopo kata ya Naisinyai wilayani humo.

Zacharia alisema kutokana na hali hiyo baadhi ya wanafunzi wanosoma kutwa kwenye shule hiyo hulazimika kutembea kila siku umbali wa kilomita 20 kwenda shule na kurudi nyumbani hivyo kuchangia kushusha kiwango cha taaluma.

Alitoa wito kwa jamii inayozunguka eneo hilo kuchangia gharama za ujenzi wa bweni la kulala wanafunzi hao kuliko kuiachia Serikali peke yake kwani wanaoteseka ni watoto wanaozunguka eneo hilo.

“Kama mlivyosema hiyo ni changamoto kwa jamii yetu kuchanga ili Serikali nayo itie mkono wake lakini hivi sasa mtakuwa mnawapa walimu kazi mbili ya kufundisha na kutoa pole watoto wanapochoka kutembea,” alisema Zacharia.

Pia,Diwani huyo alijitolea sh1 milioni na kuungana na Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai Taiko Kurian aliyechangia sh1 milioni kwa ajili ya ununuzi wa mashine ya kuweka umeme wa jua (sola) kwani shule hiyo haina nishati ya umeme.

Akisoma risala kwenye mahafali hayo,Mkuu wa shule hiyo,Emmanuel Kirenga alisema shule ya sekondari Naisinyai ilianzishwa Februari 13 mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi 101 na walimu watatu.

Mwalimu Kirenga alisema kuwa hivi sasa shule hiyo ya sekondari Naisinyai ina wanafunzi 491 wakiwemo wahitimu 103 waliomaliza kidato cha nne na wana walimu 16 na wafanyakazi wa shule sita.

Alisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabweni ya kulala wanafunzi,utoro uliokithiri,uzio unaosababisha mifugo kuingia shuleni na kuharibu mazingira na ukosefu wa nishati ya umeme.

Alimshukuru Zacharia kwa kuchangia sh1 milioni ya kununua umeme wa sola na pia alitoa shukrani kwa Elibariki Solomoni mmoja wa wazazi walio na wanafunzi shuleni hapo aliyejitolea jenereta kwa ajili ya nishati ya umeme shuleni hapo.


About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia